NA HAJI NASSOR, PEMBA

MGANGA (24) na wasaidizi wake wawili wenye miaka 15 na 16, wanaotuhumiwa kumbaka mteja wao kwa nyakati tofauti wakidai kutumwa na majini kama sehemu ya tiba, wamelazimika kurejeshwa rumande, baada ya upande wa mashtaka kutopokea mashahidi.

Mara baada ya watoa tiba hao kuwasili mahakamani hapo wakiwa chini ya ulinzi hakimu wa mahakama ya Mkoa Chake Chake Abdull-razak Abdull-kadir Ali, alipomtaka Mwendesha mashtaka kueleza hatua ya kesi hiyo.

Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa shauri hilo lipo mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza mashahidi waliobakia ingawa bado hawajawapokea.

“Mheshimiwa hakimu, shauri hili linalowakabili waganga watatu wa kienyeji, tulitarajia leo ‘jana’ tuwasikilize mashahidi wengine, ingawa hatujawapokea na tunaomba uliahirishe na kulipangia tarehe nyengine,’’alidai.

Ndipo hakimu huyo, alipokubaliana na ombi hilo na kuwataka washtakiwa hao, kurudi tena mahakamani Agosti 11 mwaka huu, kuendelea na shauri lao.

Wiki iliyopita, wakati akitoa ushahidi wake mwanamke aliyebakwa na waganga hao mwenye miaka 40, aliieleza mahakama hiyo kuwa, aliwahi kubakwa mara tatu kwa siku tofauti na mganga na wasaidizi wake, akiwa mtoni anafua, wakidai kuwa ni sehemu ya tiba ya magonjwa yanayomkabili.

Alidai, siku hiyo alipokuwa mtoni anafua, ndipo alipofuatwa na msaidizi wa mganga, mwenye miaka 16 na kumwambia ametumwa na mganga wake mkuu, wafanye tendo la ndoa, ili apone.

Awali, aliiambia mahakama hiyo chini ya Hakimu Abdull-razak Abdull-kadiri Ali kuwa, tayari kwa siku zilizopita alishawahi kubakwa na mganga wa vijana hao, wakati akiwa mtoni anafua, akidai ni sehemu ya tiba.

Mapema shahidi namba mbili mume wa muathirika huyo, alidai kuwa siku hiyo, wakati anarudi shamba, ndipo alipokuta beseni la nguo la mke wake, pembeni mwa njia inayotoka mtoni na kupatwa na wasi wasi.

Washtakiwa hao ni Hemed Ali Khamis mwenye miaka 24, mtoto mwenye umri wa miaka 16, na mwengine ni mtoto mwenye miaka 15 wote wakaazi wa Mikinduni Mgagadu Wilaya ya Mkoani.

Ilidaiwa kuwa, mtuhumiwa namba moja ambaye ni Hemedi Ali Khamis alitenda kosa siku na tarehe isiyofahamika mwezi Januari mwaka huu mjira ya saa 5:00 asubuhi kwenye mabonde ya Mikinduni Mkoani.

Ilidaiwa kuwa, akiwa kama mganga wa kienyeji alitumia nafasi yake hiyo, kumbaka mwanamke mwenye miaka 40, ambaye alitaka kumfanyia matibabu, huku akidai ametumwa na shetani wake kama ni miongoni mwa masharti ya kupona maradhi yake.

Kosa la pili, mwezi huo huo saa 3:00 asubuhi kwenye mabonde ya Mikinduni, alimbaka mama huyo akiwa na lengo la kutaka kumfanyia matibabu.

Kosa la tatu ilidaiwa kulitenda mtuhumiwa namba moja na namba mbili mwenye miaka 16, siku na tarehe isiyofahamika mwezi Machi mwaka huu saa 6:00 mchana katika mabonde ya Mgelele Mikinduni walimbaka mwanamke huyo.

Kosa la nne kwa mshitakiwa namba moja na tatu mwenye miaka 15, walilitenda mwezi huo huo saa 4:00 asubuhi mabonde ya Mgelele, bila ya halali walimbaka mwanamke huyo, ambapo kosa la tano alilitenda mtuhumiwa namba mbili pekee mwezi huo huo mwaka huu saa 1:00 asubuhi Mikinduni Mkoani alimbaka mwanamke huyo mwenye miaka 40.

Kosa jingine inadaiwa kulitenda mtuhumiwa namba tatu, mwezi huo huo saa 1:00 usiku Mikinduni Mkoani, alimbaka mwanamke huyo, ambapo kosa la saba walidaiwa kulitenda watuhumiwa namba mbili na namba tatu Aprili 10 mwaka huu saa 7:00 mchana katika mabonde ya Mgelele walimbaka mwanamke mwenye miaka 40.

Kufanya hivyo ni kosa, kinyume na kifungu cha 108 (1) (3) (d) na kifungu cha 109 (1) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018, Sheria ya Zanzibar.