NA MWANDISHI WETU

NI vugumu kuzungumzia utapeli wa kimataifa bila mtaja Mithilesh Kumar Srivastava ajulikanae pia kwa jina la umaarufu la Natwarlal.

Natwarlal ameweka kumbukumbu ya kipekee nchini India kutokana na kufanya utapeli wa aina yake ikiwa ni pamoja na kuuza majengo ya kihistoria ya Taj Mahali mara tatu.

Aliuza Red Fort mara mbili, kuuza jengo rasmi la makazi ya rais wa India liitwalo Rashtrapati Bhavan lilioko magharibi mwa kitongoji cha Raj path mjini New Delhi. Si hayo tu, bali pia tapeli huyo wa kimataifa amewahi kuuza jengo la bunge la India likiwa na wabunge 545 ndani yake.

Mithilesh Kumar Srivastava alizaliwa mwaka 1912 katika kijiji cha Siwan katika eneo la Bihar akiwa ni mtoto wa kwanza wa kiume wa mfanyabiashara aitwae Zamindar aliyemiliki shamba kubwa.

Kumbukumbu za kihistoria zinaonesha kuwa akiwa kijana mdogo alianza kuiba benki kwa kughushi saini ya jirani yake pale alipopewa pesa na jirani huyo kwenda kumuwekea benki. Hiyo ilikuwa ni kabla ya India kupata uhuru wake.

Baada ya jirani huyo kugundua kuwa zaidi ya Rupia Laki moja zametolewa katika hesabu yake ya benki, Mithilesh Kumar alikimbia katika mji huo wa Bihar na kuhamia mjini Calcutta na kuendelea na masomo na kutunukiwa shahada ya sheria.

Hivyo kabla ya kuingia katika utapeli alikuwa ni mwanasheria. Kazi ya kwanza alofanya tapeli huyo ilikuwa ni dalali wa kubadilisha fedha ambapo jaribio la kwanza la utapeli kufanywa na kijana hiyo ilikuwa ni katika mwaka 1937, pale alipojaribu kuuza tani 9 za nondo zilizokuwa zimewekwa pembeni ya barabara.

Kwa kutumia vielelezo na nyaraka bandia alizotengeneza, tapeli huyo alikwishapata mteja wa kumuuzia nondo hizo, lakini kabla ya mpango wake huo kukamilika mwenye mali hiyo aligutuka na mtu huyo alitiwa mbaroni na polisi wa mjini Calcutta na kufungwa jela.

Baada ya kutoka gerezani, Mithilesh Kumar alianzisha aina nyengine ya utapeli ambapo aliwatongoza wanawake wanaojiuza na kwenda nao katika nyumba za kulala wageni na baada ya kufika ndani aliwapa kinywaji chenye dawa ya usingizi na baada ya mwanamke huyo kulala aliwaibia kila kitu na kukimbia. Alitiwa tena mbaroni na polisi baada ya mwanamke mmoja kumjua tapeli huyo na kuripoti polisi.

Tapeli huyo hakuishia hapo, kwani baada ya kutoka gerezani alibuni mbinu mpya ya utapeli ambapo alikwenda katika kituo cha treni na iwapo ataona mzigo wenye thamani kubwa alitumia nyaraka bandia alizoghushi na kwa kutumia utaalamu wake wa sheria, fedha na benki alifanikiwa kuwatia mtegoni watu kadhaa walonunua mizigo hewa hiyo.

Mithilesh Kumar kwa kutumia vielelezo na nyaraka kadhaa bandia alidai kuwa yeye alikuwa na mfanyabiashara mwenzake aitwae “Natwarlal” ambaye hakuwepo ndio maana tapeli huyo akapewa jina la utani “Natwarlal.

Kutokana na kubobea katika mbinu za utapeli, Mithilesh Kumar aliwatia mtegoni na kuwaibia mamia ya watu kwa kuchangisha michango hewa, kukusanya kodi na kutumia zaidi ya majina hamsini bandia ili kuficha utambulisho wake.

Pamoja na yote hayo, Natwarlal alikuwa bingwa wa kuigiza na kughushi saini za watu mbalimbali mashuhuri ambazo alitumia katika kufanikisha utapeli wake.  Kwa kutumia saini hizo bandia za maafisa waandamizi wa serikali ndipo alipofanikiwa kuuza majengo ya serikali ikiwemo bunge la India.

Katika hali isiyo ya kawaida iliyoshangaza wengi kutokana na kuwa ngwiji wa upateli, Bwana huyo alifanikiwa kuyaibia makampuni makubwa ya India ikiwemo kampuni ya kutengeneza magari ya TATA, kampuni ya Birlas inayoendesha biashara mbalimbali na kampuni maarufu ya biashara ya Dhirubhai Ambani yenye mtandao mkubwa wa biashara mbalimbali nchini India na barani Asia.