MNAMO Juni 29 mwaka huu serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliruhusu kufunguliwa skuli ili watoto waendelee na masomo baada ya kufungwa kwa takriban miezi mitatu kutoka na mripuko wa maradhi ya corona.

Wakati serikali inaruhusu kufunguliwa kwa skuli hizo, ikasisitiza lazima miongozo ya wataalamu afya ifuatwe kikamilifu ili kuepuka maambukizi ya maradhi ya corona kwa wanafunzi.

Miongoni mwa mikakati ambayo skuli ilitakiwa itekelezwe ni suala zima la wanafunzi kunawa mikono kwa maji yenye kutiririka sambamba na wanafunzi wakae kwa kupeana nafasi.

Jamii ilikuwa na matumaini makubwa kwamba tangazo la serikali la kufunguliwa skuli lingekwenda sambamba na kufunguliwa kwa madrasa ambazo watoto wetu wanapata fursa ya kujifunza kitabu kitukufu cha kur-ani.

Wakati tangazo lakufunguliwa skuli likitekelezwa serikali kupitia Ofisi ya Mufti ikasisitiza kuwa madrasa zinazotoa fursa watoto kujifunza kur-ani zitaendelea kufungwa, hapo ndipo jamii iliposhusha malalamiko mengi.

Wapo waliosema maneno mazito ya kashfa pengine hata si vyema kuyaandika kwenye tahariri hii wakiikashifu Ofisi ya Mufti kwanini imekubali kuendelea kufungwa madrasa na kukubali skuli kufunguliwa.

Kwa wakati wote huo watu wakilalamika Ofisi ya Mufti ilikuwa kimya kama vile haielewi kile kinacholalamikiwa na jamii, hivyo mnamo Julai 17, serikali ikatangaza kufunguliwa kwa madrasa.

Siku chache baada ya kufunguliwa madrasa, Ofisi ya Mufti ikaeleza sababu za kuchelewa kufunguliwa kwa madrasa ambapo moja ilielezwa kwamba vyuo vingi havina mazingira rafiki hasa vyoo.

Aidha madarasa zetu nyingi zinamsongamano wa watoto jambo ambalo si rahisi kutekelezwa agizo la wanafunzi kukaa mbalimbali na hali ikiwa hivyo kuna uwezekano wa maambukizi ya corona.

Kimsingi Ofisi ya Mufti ilikuwa na sababu za msingi, lakini ilishindwa kuzieleza kwa wakati ndio maana wamejikuta kwenye hatua mbaya kiasi cha kufikia watu kutoa kashafa na matusi.