NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

RAIS Mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mzee Benjamin Mkapa ataendelea kukumbukwa kwa ujasiri, uwajibikaji na kujituma ndani na nje ya Tanzania.

Hayo aliyasema jana nyumbani kwake Masaki jijini Dar es Salaam, wakati viongozi mbali mbali walipofika nyumbani hapo kutoa salamu za pole na kusaini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha mzee Mkapa kilichotokea usiku wa kuamkia Ijumaa.

Akizungumza mara baada kusaini kitabu hicho, katibu mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally alisema marehemu mzee Mkapa kati ya mambo ambayo atakumbukwa ni kuijengea misingi imara ya uchumi Tanzania.

Katibu huyo alisema nje ya Tanzania, marehemu mzee Mkapa mara baada ya kustaafu urais alijishughulisha na masuala ya usuluhishi wa migogoro hasa kwa nchi za Afrika Mashariki.

Alisema mzee Mkapa aliiwakilisha vizuri CCM katika awamu zote mbili alizokaa madarakani kwa kutekeleza kwa vitendo ilani ya Chama cha Mapinduzi na kupeperusha vizuri bendera na kusababisha kupata ushindi kwa asilimia 60 wakati wa uchaguzi.

Alieleza marehemu mzee Mkapa alikijenga vyema chama, kupiga vita rushwa na kusimama katika uadilifu na uwajibikaji wa kutoa maamuzi hali ambayo ilimsaidia mrithi wake rais Mstaafu wa awamu ya nne, Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kupata ushindi kwa kura asilimia 80 katika uchaguzi mkuu.

Alisema Rais wa kwanza Tanzania Mwalimu Julius Nyerere aliwatengeneza marais wawili akiwemo marehemu Mkapa na Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na kukiletea ushindi chama na hadi sasa kunaendelea kushika hatamu ya madaraka.

Naye aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema alikaa na marehemu Mkapa kwa miaka 38 alipofanya kazi katika serikali, Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alisema anaungana na watanzania wote pamoja na kumpa pole rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kwa msiba huu mkubwa uliotokea ghafla.

Alifafanua kuwa, katika CCM aliweza kujituma sana katika kusimamia ilani ya chama hicho na kujenga nidhamu na kuwa mfuatiliaji mzuri wa malengo aliyoyapanga yanafikiwa kwa ufanisi.

Akigusia suala la uchaguzi mkuu kufanyika bila ya kuwepo mzee Mkapa, alisema uchaguzi wowote ni mgumu kwa sababu kura ya mtu ipo ndani ya moyo wake na haipo usoni.

Aidha rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume nae alifika nyumbani kwa marehemu Mkapa Masaki kwa ajili ya kutoa mkono wa pole na kuweka saini katika kitabu cha maombolezo.