Wampitisha Dk. Magufuli asilimia 100

Dk. Hussein atambulishwa

Taarifa za utekelezaji za serikali zawasilishwa

Ilani mpya, marekebisho ya katiba yapitishwa

Samia mgombea mwenza tena

SAIDA ISSA NA RAMADHAN MAKAME, DODOMA

WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wamelithibitisha jina la Dk. John Pombe Magufuli kuwa mgombea wa chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika baadae mwaka huu.

Kwenye hafla hiyo iliyofanyika jana katika ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete uliopo Dodoma, wajumbe hao walimpitisha Dk. Magufuli kwa kumpigia jumla ya kura 1,822 sawa na asilimia 100.

Dk. Magufuli alikuwa mgombea pekee aliyejitokeza kuchukua fomu na kupitishwa na halmashauri kuu ya CCM kuwania awamu ya pili ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika mkutano huo, alitambulishwa Dk. Hussein Mwinyi ambae aliibuka mshindi kwenye kinyang’anyiro cha watu 31waliojitokeza kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar kupitia chama hicho.

Hapo juzi halmashauri kuu ya CCM ilimpitisha Dk. Mwinyi kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar baada ya kupata kura 129 dhidi ya kura 19 za Dk. Khalid Salum  Mohammed na kura 16 za Shamsi Vuai Nahodha.

Akizungumza baada ya kuthibitishwa na mkutano kuwa mgombea pekee na ikiwa ni hotuba yake ya kuufunga mkutano huo, Dk. Magufuli aliwashukuru wajumbe wa mkutano huo kwa kumchagua kwa asilimia 100 na kumpitisha kuwa mgombea wa urais.

Alisema hakutegemea na kwamba kura alizozipata ni deni na malipo yake ni kuwatumikia wananchi wa Tanzania.

 “Kura nilizozipata leo, zisinipe kiburi, zikaniongezee nguvu kuwatumikia watanzania,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kuwapongeza wanaCCM waliomdhamini ambapo zaidi ya watu milioni moja walijitokeza na kwamba hali hiyo inaonyesha deni kubwa alilonalo katika kuwatumikia watanzania.

Alisema Tanzania ni nchi iliyojaaliwa kuwa na kila aina ya rasilimali na kwamba CCM itahakikisha inaleta mabadiliko kwa kuwapatia wananchi maendeleo na kwamba watu watakaoteuliwa wana wajibu wa kuwatumikia watanzania.

“Mmenipa ushindi wa asilimia 100, msitarajie tutapata ushindi wa asilimia 100, mkafanye kazi ili tuweze kupata ushindi kwa kura za urais, kura za wabunge na madiwani,”alisema.

Aliwapongeza wanaCCM waliogombea urais wa Zanzibar na kusema kwamba ni watu wa pekee hasa kwa kuelewa kuwa watu 31 lakini anayetakiwa ni mmoja tu.

“Niseme kuhusu Hussein Mwinyi, yeye ni tofauti na watoto wengine wa wakubwa, ni mtu ambaye hakutumia ukubwa wa baba yake ni mtu mwenye heshima ni mtu tofauti sana,” alisema.

“Nataka niwape siri moja sijawahi kuisema lakini leo naisema, wakati nilipokuwa namchagua mgombea mwenza nililetewa watu wawili Mwinyi na Samia na kama Samia angekuwa si mwanamke, Mwinyi angekuwa makamu wa rais,” alisema.

Alisema wakati alipoikosa nafasi hiyo hakulalamika alizidisha upole na kutekeleza vyema wajibu wake na kwamba hata alipopewa nafasi ya waziri wa ulinzi alifanyakazi zake vizuri.

Alisema Dk. Mwinyi ni damu mpya aliyezaliwa baada ya mapinduzi ya 1964 na kwamba kama atachaguliwa Zanzibar itapaa zaidi na kwamba kuchaguliwa kwake sio usultani.

Awali akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo, Dk. Magufuli alisema mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ni matokeo ya juhudi za viongozi wa CCM walivyosimamia vyema ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015 – 2020.

Alisema mambo yaliyofanyika ni mengi na watanzania wote na hata nje ya nchi wanaelewa na ni mashahidi wa maendeleo yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitano.

Alisema ilani mpya ya uchaguzi iliyopitishwa jana na wajumbe wa mkutano huo inaeleza mikakati mingine itakayotekelezwa yenye maslahi kwa watanzania.

“Nyinyi ndio mlioiweka Tanzania kwenye ramani, mafanikio haya pia yamechangiwa na watangulizi wangu akiwemo Mwl. Nyerere, mzee Ali Hassan Mwinyi, mzee Mkapa na mzee Kikwete, wazee wetu hawa wote wamefanya kazi nzuri,”alisema.

Alifahamisha kuwa maendeleo hayana chama, hivyo watanzania washikamane kuijenga nchi yao na kila linalofanyika ni kwa ajili ya watanzania. “Nimechukua fomu ili tukayamalize yale yaliyobakia, nikashirikiane na nyinyi kwa ajili ya kuwaletea maendeleo watanzania wote,” alisema.

Akiwasilisha taarifa yenye kurasa 134 ya utekelezaji ya miaka mitano iliyowasilishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaaliwa, alisema aliwashukuru watanzania kwa ushirikiano wa ujenzi wa nchi yao na kuwataka wajumbe wakisome kitabu hicho.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, aliwasilisha taarifa yenye kurasa 133 iliyoelezea mafanikio ya miaka 10 yaliyotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na baadae wajumbe kuipitisha taarifa hiyo.

Zoezi jengine lililofanyika katika mkutano huo, ni kufanya mabadiliko ya katiba ambayo yatawawezesha Wenyeviti wa mashina wa chama hicho kuwa na uwezo wa kupiga kura kuwachagua viongozi wa ngazi za wadi na kata.

Aidha mkutano huo uliridhia na kuipitisha ilani mpya ya uchaguzi wa chama hicho (2020-2025), ambayo itanadiwa kwenye kampeni za uchaguzi mkuu.

Viongozi mbalimbali walialikwa kwenye mkutano huo wakiwemo waliowahi kuwa wenyeviti, makamu wenyeviti, makatibu wakuu, waliowahi kuwa viongozi wa jumuiya za chama.

Aidha CCM iliwaalika kwenye mkutano huo viongozi wa vyama rafiki kutoka nchi mbalimbali za Afrika na nje ya Afrika ikiwemo Burundi, Vietnam, Sudan Kusini, Msumbiji, Cuba, Afrika Kusini na DRC.

Akizungumza katika hafla hiyo Balozi wa China nchini Tanzania, alisema chama cha CPC cha China kinajivunia kwa dhati ushirikiano ulionao na chama cha Mapinduzi.

Naye mwakilishi wa vyama vya upinzani nchini Tanzania, Prof. Ibrahim Lipumba kutoka CUF, alipongeza kualikwa na kuomba ziwepo kampeni za kistaarabu na watu washindane kwa hoja.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama cha TLP, Augustine Mrema, alisema halmashauri ya chama chake ilipitisha azimio la kumuunga mkono Dk. John Pombe Magufuli kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika baadae mwaka huu.

Kwa niaba ya mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa, alisema hakuna ubishi nchi imetulia na maendeleo yanakwenda kwa kasi na kutaka kasi isipungue.

Naye Abrahman Kinana akizungumza katika mkutano huo kwa niaba ya waliokuwa makatibu wakuu wa CCM, aliwaomba wajumbe wahakikishe wanakwenda kumtafutia kura John Pombe Magufuli katika uchaguzi mkuu ujao.

Kwa niaba ya marais wastaafu, Rais wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano, Ali Hassan Mwinyi, aliwaomba wajumbe wa mkutano huo na watanzania wote kujenga nchi yao.