KINSHASA, DRC

RAIS wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi amemteuwa mkuu mpya wa jeshi kuchukua nafasi ya Jenerali John Numbi.

Numbi na mrithi wake mteule, Jenerali Gabriel Amisi Kumba, wako chini ya vikwazo vya Marekani na Umoja wa Ulaya kwa ukandamizaji na dhuluma dhidi ya viongozi wa upinzani na waandamanaji chini ya rais wa zamani Joseph Kabila.

Ofisi ya Tshisekedi haijatoa sababu ya mabadiliko hayo. Mwezi uliopita umeshuhudia ongezeko la mivutano ndani ya serikali ya muungano kati ya wafuasi wa Tshisekedi na wale wa Kabila, ambao wana nguvu nyingi kupitia wingi wao bungeni, wanadhibiti wizara nyingi za serikali na wana ushawishi jeshini.

Mpaka sasa, Kumba alikuwa naibu wa Numbe na kiongozi wa operesheni za kimpaka za Jeshi la Congo. Wote walipandishwa vyeo na Kabila katikati ya mwaka wa 2018.