KHAMISUU ABDALLAH NA MWAJUMA JUMA

MTU mmoja aliyetambulika kwa jina la Hija Suleman anaekisiwa kuwa na umri wa miaka 38 hadi 40 mkaazi wa Mwera amefariki dunia katika ajali ya moto.

Akizungumza na vyombo vya habari Kaimu Kamanda Mkoa wa Mjini Magharibi, Simon Pasua alisema ajali hiyo ilitokea jana majira ya saa 8:00 katika hifadhi ya mafuta ‘depot’ ya PUMA iliyopo Mtoni Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema, marehemu huyo ni dereva wa kampuni ya Bachu na chanzo cha moto huo kilitokana na gari iliyokuwa ikiweka mafuta ya taa katika tenki kuripuka.

Aidha alisema Jeshi la Polisi lilishirikiana na Kikosi cha Zimamoto na Uokozi kuhakikisha linaudhibiti moto huo na wamefanikiwa bila kusababisha madhara zaidi.

Pasua alisema Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi wa tukio hilo na mwili wa marehemu umeshapelekwa katika hospitali kuu ya Mnazimmoja kwa uchunguzi.

“Bado mapema kueleza chanzo cha tukio hili tunaendelea na upelelezi, lakini moto umedhibitiwa na eneo lililoripuka limefungwa,” alisema.

Kamishna wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar, Ali Abdalla Malimusi alisema kikosi hicho kimefika kwa wakati na kuweza kuudhibiti moto huo ili usiendelee kuleta madhara.

“Tunashukuru tumefika katika muda muafaka na moto huu ulisababishwa na mafuta ya taa na ingekuwa petrol basi maafa yangekuwa makubwa,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Kamisheni ya kukabiliana na maafa Zanzibar, Makame Khatib Makame alisema tathmini halisi ya tukio bado haijajulikana na kukipongeza kikosi KZU kwa kuweza kuudhibiti moto huo na kuepusha maafa.

Hata hivyo, aliziomba kampuni zinazosimamia maeneo hayo kuweka mifumo madhubuti ya kuzuia majanga pale yatakapojitokeza.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘A’ ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama alisifu juhudi zilizochukuliwa na kikosi hicho na kuwatoa hofu wananchi juu ya janga lililotokea.