LONDON, England

KOCHA Mkuu wa Tottenham Hotspur Jose Mourinho amemwambia mwenyekiti wa timu hiyo Daniel Levy, kuwa asiruhusu kumuuza mshambuliaji wake Harry Kane msimu huu.

Imekuwa ikielezwa kuwa Spurs ipo kwenye mpango wa  kumuuza Kane raia wa England kutokana na timu kuyumba kidogo kwa upande wa uchumi kutokana na janga la Virusi vya corona.

Pia, Mourinho amesisitiza kuwa ni lazima timu hiyo kufanya maboresho kidogo kwenye kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao pale dirisha la usajili litakapofunguliwa.

Mshambuliaji huyo ametupia jumla ya mabao 17 na kutoa pasi mbili za mabao akiwa amecheza jumla ya dakika 2,499 akiwa na wastani wa kutupia kila baada ya dakika 147.

Mourinho amesema:”Naona kwamba sio jambo zuri kumuuza mchezaji muhimu kama Kane, ila kwenye kikosi chetu lazima tufanye maboresho kidogo, maboresho makubwa yatahitaji fedha nyingi.”