PARIS,UFARANSA
MRIPUKO mpya wa virusi vya corona barani Ulaya umepiga kengele ya hatari kwa watu wa bara hilo huku viongozi wa nchi mbalimbali wakisisitiza udharura na kufuatasheria za afya.
Msemaji wa Shirika la Afya Dunia (WHO) kanda ya Ulaya,alisema maambukizi ya virusi vya corona barani humo yaliongezeka katika wiki mbili zilizopita na kuongeza kuwa,mripuko mpya wa ugonjwa wa COVID-19 katika baadhi ya nchi za Ulaya unatokana na kupuuzwa masharti na sheria ya afya ya kipindi cha corona.
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Ufaransa Jean Castex aliwaasa wananchi wa nchi hiyo wasifanye safari katika jimbo la Catalonia la kaskazini mwa Uhispania baada ya Serikali ya nchi hiyo kufunga mikahawa na klabu za usiku kutokana na ongezeko la maambukizi ya corona.
Pia Serikali ya Uingereza iliwaamuru raia wote kuvaa barakoa wanapotoka nje kwa ajili ya kununua bidhaa madukani,masokoni na kwa ajili ya shughuli za Benki.
Nchini Austria pia Serikali iliwaamuru watu wote kuvaa barakoa wanapotoka nje kwa ajili ya shughuli mbalimbali kama masokoni, madukani, idara za Serikali, kwenye vyombo vya usafiri wa umma, Hospitali na kadhalika.
Hatua kama hizo pia zilitangazwa katika nchi nyengine kadhaa za Ulaya.
Bara la Ulaya ndilo linaloongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu walioaga dunia kutokana na virusi vya corona.
Hadi sasa zaidi ya watu milioni tatu wameambukizwa virusi vya corona barani humo na zaidi ya nusu yao wako katika nchi za Uingereza, Uhispania, Italia na Russia.