ADDIS ABABA, Ethiopia
MAANDAMO makubwa yamezuka nchini Ethiopia kufuatia mauaji ya mwanamuziki, Hachalu Hundessa, aliyepata umaarufu kutokana na nyimbo zake za kisiasa.

Watu wawili wamefariki wakati wa maandamano hayo katika mji mmoja, madaktari wameiambia BBC.

Nyimbo za Hachalu zilikuwa zinaangazia haki ya jamii ya Oromo na zilitumiwa katika msururu wa maandamano yaliyochangia kuondoka madarakani kwa Waziri Mkuu aliyekuwepo wakati huo.

Muimbaji huyo aliyekuwa na umri wa miaka 34 alikuwa amesema kwamba amepokea ujumbe wa kumtishia maisha.
Katika moja ya nyimbo zake maarufu, aliimba: “Msisubiri kupata msaada kutoka nje, hiyo ni ndoto ambayo sio ya kweli. Amka, ujiandae kupambana, kwa sababu ni wewe uko karibu na kasri.”

Mwanamuziki huyo aliwahi kufungwa jela miaka mitano akiwa na umri wa miaka 17 kwa kushiriki katika maandamano.
Wengi kama yeye walikimbilia uhamishoni kwa kuhofia kuteswa, lakini, Hachalu aliamua kubakia nchini kuwahimiza vijana wapiganie haki yao.

Maelfu ya mashabiki wake walielekea katika hospitali ya Addis Ababa ambako mwili wa muimbaji huyo ulipelekwa usiku wa Jumatatu.

Kwao, alikuwa sauti ya kizazi ambacho kinapinga unyanyasaji wa miongo kadhaa wa serikali dhidi yao.

Polisi walitumia vitoa machozi kutawanya makundi ya watu huku milio ya risasi ikisikika jijini Addis Ababa.

Waziri Mkuu, Abiy Ahmed, alituma rambi rambi zake katika mtandao wake wa ‘Twitter’ akisema, Ethiopia imepoteza kiungo muhimu na kutaja tungo zake kuwa nzuri.

Oromo ni kabila kubwa zaidi nchini Ethiopia, ambalo kwa muda mrefu limekuwa likilalamikia kutengwa kisiasa na kiuchumi.