KITENGO cha Maadili (AIU) cha Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kimempiga marufuku mkimbiaji  Alex Korio Oloitiptip kushiriki mashindano kwa miaka miwili kwa kukiuka kanuni zinazodhibiti matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

Korio, 30, alipigwa marufuku hiyo Mei mwaka huu baada ya kubainika kwamba hakujitokeza kupimwa mara tatu ili kubaini iwapo aliwahi kutumia dawa haramu za kusisimua misuli.

Ingawa alipewa nafasi ya kujitetea, ushahidi aliowasilisha haukusadikisha wana jopo wa AIU.

Taarifa ya AIU imesema, Korio alikosa kufanyiwa vipimo vya afya mara tatu mfululizo chini ya kipindi cha miezi 12.

Hilo ni kosa ambalo humpa mwanariadha yeyote marufuku ya moja kwa moja.

Isitoshe, alikataa kujibu barua alizotumiwa na kitengo hicho wala kutoa maelezo yoyote alipotakiwa kueleza sababu ya kushindwa kufanyiwa vipimo.