NA KHAMISUU ABDALLAH

UONGOZI wa Jimbo la Malindi, umekabidhi vitu mbalimbali kwa wananchi wa jimbo hilo, ili waweze kuvitumia katika shughuli zao za kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Akikabidhi vitu hivyo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini kichama Talib Ali Talib, alisema vitu hivyo vilivyokabidhiwa itakuwa chachu ya kuimarisha maendeleo ya jimbo hilo na maeneo mengine.

Alisema, uongozi wa jimbo umesimama imara utekelezaji wa ilani ya chama kwa kuimarisha miundombinu ya elimu, barabara na maji na huduma nyengine, ili kuwaondoshea usumbufu wananchi na waweze kuitumia kwa urahisi.

Mwenyekiti huyo, aliwataka wananchi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu kuhakikisha wanawachagua viongozi wa chama hicho katika nafasi ya Ubunge, Uwakilishi na Udiwani, ili wazidi kuletewa maendeleo.

Alisema, jimbo hilo linaongozwa na mwakilishi lakini imepiga hatua kubwa ya kimaendeleo kutokana na kiongozi huyo kujitoa kwa hali na mali katika kuwatumikia wananchi wake.

Nae, Mwakilishi wa Jimbo hilo, Mohamed Ahmada Salum, alisema ataendelea kushirikiana na wananchi pamoja na wanachama wa jimbo hilo ili kuhakikisha wanakipatia ushindi chama katika ngazi zote.