NA SAIDA ISSA, DODOMA

MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Semistocles Kaijage ametangazia kwa wenye sifa na watakaopendekezwa na vyama vyao vya siasa vyenye usajili wa kudumu kujitokeza kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano, ubunge na udiwani.

Itakumbukwa kuwa mnamo Julai 21, NEC ilitangaza ratiba ya uchaguzi mkuu ikionyesha kuwa uteuzi wa kiti cha rais, ubunge na udiwani utafanyika kuanzia Agosti 25 mwaka huu.

Kauli hiyo iliyolewa jana jijini Dodoma katika ofisi za Tume zilizofunguliwa mwanzoni mwa wiki hii na Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli.

Jaji Semistocles alisema fomu kwa ajili ya wagombea kiti cha urais zitatolewa kuanzia Agosti 5 hadi 25 mwaka huu katika ofisi za tume hiyo.

Alisema kuwa kwa upande wa majimbo ya uchaguzi tume chini ya ibara ya 74 ya katiba ya jamhuri ya Muungano Tanzania imepewa jukumu la kuchunguza mipaka na kuigawa Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge.

“Tume inatumia fursa kutangaza mabadiliko ya majina kwa majimbo ya uchaguzi mwaka huu ambapo jimbo la Chilonwa limebadilishwa jina na kuwa jimbo la Chamwino, jimbo la Mtera limebadilishwa jina na kuitwa Mvumi na jimbo la Kijitoupele lililopo wilaya ya Magharibi ‘B’ limebadilishwa jina linaitwa Pangawe”, alisema.

Alisema idadi ya majimbo ya uchaguzi yanabakia kuwa 264 kama ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ambapo Tanzania bara ina idadi ya majimbo 214 na Tanzania Zanzibar ina majimbo 50 na jumla ya kata 3,956 za Tanzania bara zitafanya uchaguzi wa madiwani mwaka huu.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa ofisi za NEC, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli alisema kuwa bilioni 16.8 zimetumika katika ujenzi wa jengo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Alisema kujengwa ofisi hizi hapa Dodoma kutawarahisishia wadau na viongozi wa uchaguzi katika kazi kwa sababu hapa ndipo makao makuu ya nchi na Ofisi za Tume ya uchaguzi Taifa zimejegwa pia ni katikati ya nchi.