NA MWANDISHI WETU

IKIWA watanzania wako katika maombolezi ya Rais wao mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Willium Mkapa, watamkumbuka kwa mambo mengi mema na muhimu kwa nchi ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania aliyoyafanya wakati wa uongozi wake.

Ni wazi kuwa hataka kama yatatajwa yote basi hayatoweza kumalizika kwa leo lakini cha kusema kuwa hakuna budi kumshukuru na kumtakia malazi mema peponi huku akiendelea kukumbukwa daima.

Juzi akitangaza taarifa ya mazishi ya Mzee Mkapa, waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema nchi imempoteza kiongozi shupavu na kwamba ameacha pengo kubwa.

Pamoja na mambo mengine lakini Mzee Mkapa alikuwa ni kiungo muhimu katika kuuimarisha uchumi wa Tanzania enzi za utawala wake sambamba na kuiweka nchi katika hali ya amani licha ya wakati huo kuwa katika vuguvugu kubwa la mfumo wa vyama vingi na kuwa katika uchaguzi mkuu uliokumbwa na mzozo.

Mbali na ushujaa alioonesha Tanzania kwa nyanja mbalimbali kama kiuchumi na kisiasa lakini Mzee Mkapa pia alionekana na kuwa mtu wa busara kubwa hasa baada ya kustaafu urais jambo ambalo alipelekea kuchaguliwa na jumuiya za kimataifa kama kuwa mpatanisha wa migogoro hasa kwa nchi jirani za Kenya na Burundi.

Kwa mfano wachambuzi wa mambo ya kisiasa walimtaja Mkapa kama mpatanishi na kwa pamoja walizungumzia mchango wake kwenye upatanishi wa mgogoro wa kisiasa wa Kenya uliotokana na Uchaguzi Mkuu wa Desemba mwaka 2007 ulioiweka nchi hii katika hatihati ya kuingia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Mkapa, kwa kushirikiana na Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa (UN), Koffi Annan ambae nae kwa sasa ni marehemu na Graca Machel kwa kutumia mwamvuli wa Kundi la Viongozi Mashuhuri wa AU -walifanikiwa kurejesha mahasimu wa kisiasa wa Kenya mezani na kuleta amani katika kipindi cha takribani siku 40 tu.

Aidha Ni Mkapa huyohuyo ambaye ndiye alikabidhiwa jukumu la kuleta amani miongoni mwa pande zilizokuwa zikizozona nchini Burundi na viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki (EAC).

Ni juhudi hizo ndizo zilizofanikisha kufanyika kwa uchaguzi wa Burundi uliofanyika Mei mwaka huu.

Mzee huyo wa busara ambae aliiongoza Tanzania kati ya mwaka 1995 hadi mwaka 2005 wakati anaingia madarakani, Rwanda ndiyo kwanza ilikuwa imetoka katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 yaliyosababisha mauaji ya zaidi ya watu milioni 1 katika taifa hilo dogo linalopakana na Tanzania.