NA MWANDISHI WETU
BENKI ya NMB imekuwa benki bora nchini Tanzania kwa mara ya nane mfululizo baada ya kuzibwaga benki zingine 40.
Tuzo
hiyo ilitolewa na Euromoney, ambalo ni jarida la kimataifa la masuala ya kifedha
linaloongoza duniani lenye makao makuu yake jijini London, Uingereza.
Tuzo hiyo inaonyesha kuwa benki ya NMB ni zaidi ya taasisi inayotoa huduma za
kifedha na kuwa kichocheo muhimu cha mabadiliko ya kiuchumi kupitia utoaji
huduma za kibenki kwa njia ya kidigitali.
Akizungumza wakati wa kukabidhiwa tuzo hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi
ya Benki ya NMB, Dk. Edwin Mhede, alisema baada ya Tanzania kufikia uchumi wa
kati, NMB inaahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu ili kuchangia zaidi
katika ukuaji wa uchumi kwenda katika hatua ya juu zaidi.
Kwa
upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, alisema:
“Leo hii tunajulikana kama benki imara zaidi, yenye huduma za ubunifu wa
kiteknolojia. Tumedhamiria kuwa zaidi ya taasisi ya huduma ya fedha kwa
kuendelea kuchochea mabadiliko ya kiuchumi katika nchi yetu na kuimarisha
maisha ya Watanzania wenzetu kwa kutoa huduma zinazowafaa na kukidhi mahitaji
na mipango yao.”
Tuzo hiyo hutolewa kwa kuzingatia vigezo kadhaa kwa benki zilizopendekezwa
ukiwamo ufanisi wa hesabu za fedha na utendaji kwa ujumla, mkakati wa huduma za
kidijitali, huduma jumuishi za fedha, usalama wa huduma za kimtandao na wajibu
wa benki kwa jamii inayoihudumia.
Vigezo vingine vilivyotumika ni mtaji wa benki, mapato yatokanayo na biashara ya hisa, mapato yatokanayo na mali za kampuni, pato litokanalo na riba, uwiano wa fedha na gharama za uendeshaji, kiwango cha amana za wateja, Kiwango cha Mikopo katika soko, Uwiano kati ya mikopo na amana za wateja, uwiano wa mikopo chechefu, uwiano wa hasara itokanayo na mikopo chechefu.
Akizungumzia mchakato wa kumpata mshindi wa tuzo ya benki bora nchini, Mhariri wa Jarida la Euromoney, Clive Horwood alisema: “Tunaendelea kuzitambua taasisi bora zaidi katika kila nchi zinazotoa huduma za fedha.”
“Kwa kila mwaka, ukubwa ni muhimu lakini sio kigezo muhimu zaidi. Faida ya benki husika ni muhimu kama ilivyo uwezo wa kuthibitisha uwezo wa kukua, ufanisi wa kiutendaji ikilinganishwa na washindani wake sokoni na uwezo wa kukabili mazingira ya soko yanayobadilika pamoja na kukidhi mahitaji ya wateja,” alisema.