NA ASIA MWALIM

KATIBU wa Mufti kuu Zanzibar Khalid Mfaume Ali, amewataka walimu wa madrasa na darsa za watu wazima kuvuta subira wakati utaratibu mpya ukiandaliwa kwa ajili ya kuzifungua madrasa na darasa za watu wazima.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na muandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Mazizini Mjini Unguja, ambapo alisema kuna umuhimu wa kuangalia suala zima la afya kabla ya kuzifungua darasa hizo.

Alisema licha ya kuwa na malamiko mengi kwa baadhi ya walimu hao kuhusiana na taarifa hiyo, inawapasa kusubiri tamko rasmi la serekali kuhusu muongozo utakaoweza kuziongoza madrasa za kur-ani na darasa za watu wazima kuendelea na masomo hayo kama ilivokua awali. 

Aidha aliwasisitiza walimu hao kuendelea kufanya kazi kwa mashirikaono na ofisi hiyo, kwani ofisi hiyo inafanya kazi zake kwa maslahi ya waislamu. 

Wakati wakizungumza na Zanzibar leo katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar baadhi ya walimu walisema taarifa hiyo imekwenda kinyume na maagizo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein wakati akivunja Baraza la tisa la Wawakilishi. 

Walisema, wakati Rais Shein, anafunga baraza hilo alitoa kauli ya kufungua shughuli zote za kijamii ikiwemo sherehe za harusi, skuli na mambo mengine.