PARIS,UFARANSA

MAHAKAMA  ya rufaa nchini Ufaransa imekataa ombi la kufungua tena uchunguzi wa mauaji ya 1994 ya rais wa Rwanda Juvenal Habyarimana ambayo yalisababisha mauaji ya kimbari ya watu 800,000. 

Mawakili wa familia za waliokufa wakati ndege ya Habyarimana ilipodunguliwa chini,watawasilisha pingamizi dhidi ya uamuzi huo wa mahakama kuu ya Ufaransa. 

Mahakama ya rufaa ya mjini Paris ilitakiwa kutathmini tena uamuzi wake wa mwaka 2018 wa kutupilia mbali uchunguzi dhidi ya washiriki tisa na wanachama wa zamani wa Rais Paul Kagame katika kesi hiyo ambayo ilihatarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili. 

Ndege iliyokuwa imembeba Habyarimana,ambaye ni Mhutu, ilidunguliwa huko Kigali mnamo Aprili 6, 1994, na kusababisha mauaji ya siku 100 yakiwalenga zaidi watu wa kabila la Tutsi, lakini pia baadhi ya Wahutu wenye msimamo wa wastani.