Lengo kushajihisha kujiajiri kupitia sekta ya utalii

NA MWANDISHI WETU

SI wanaanchi wengi wanaoifahamu taasisi isiyo ya kiserikali ijulikanayo kama ‘The Panje Project’ (TPP), ukiachilia mbali Mkoa wa Kaskazini Unguja hasa kijiji cha Nungwi, ambako ndio taasisi hiyo kwa kiasi kikubwa inakotekeleza majukumu yake na katika baadhi ya shehia za mkoa huo.

Taasisi hiyo iliasisiwa 2011 na jukumu lake kubwa ni kuhakikisha inasaidia jamii katika kuipatia elimu ambayo itawawezesha vijana kujielewa na kujipatia ajira kwenye soko la utalii ambayo ndio shughuli kubwa inayofanywa katika eneo la Nungwi, ukizingatia kuwa wenyeji wengi hawapati fursa katika sekta ya utalii kutokana na elimu yao kuwa chini.

Kama tunavyoelewa Zanzibar ni visiwa ambavyo kwa kiasi kikubwa uchumi wake unategemea sekta ya utalii ambao ina changia zaidi ya asilimia 27 ya pato la taifa na ni sekta yenye kuipatia fedha nyingi za kigeni serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Pamoja na sekta ya utalii kuwa muhimu katika kupunguza tatizo la ajira hapa nchini, kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kwamba vijana wengi hasa wazawa wanajikuta nje ya ajira kutokana na uwezo wao mdogo wa kielimu.

Nungwi kama moja wapo ya vijiji vilivyopiga hatua kubwa ya utalii, vijana wenyeji wa kijiji hicho wamejikuta wakiwa nje ya soko la ajira kwenye utalii kubakia kama watazamaji.

Bodi ya Panje iligundua kuwa tatizo la ajira kwa vijana wa Nungwi kwenye sekta ya ajira ni uwezo mdogo wa kielimu, hivyo suluhisho ni kuwaongezea uwezo ili wawe washiriki kikamilifu kwenye sekta hiyo.

Meneja wa mradi wa Panje Project, Bakhtim Marshed, alisema kutokana na kukua kwa sekta ya utalii katika kijiji hicho hasa uwepo wa hoteli pamoja na mikahawa kuliongeza mahitaji ya wafanyakazi, lakini ilikuwa vigumu sana kwa wenyeji wa Nungwi kupata ajira kwenye sekta ya utalii.