NA MADINA ISSA

HOTELI ya Park Hyatt Zanzibar imefungua tena huduma zake baada ya kusitishwa kwa zaidi ya miezi minne kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

Meneja wa hoteli hiyo, Nicolas Cedro, alisema kufunguliwa tena kwa hoteli hiyo kunatokana na kupungua ugonjwa huo na serikali kuruhusu tena shughuli za utalii.

Aidha alisema pamoja na ugonjwa huo kudhibitiwa lakini wamezingatia utoaji huduma kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya na serikali.

Aliwahakikishia wageni watakaofika hoteli hiyo usalama wa kutosha kwa sababu wamezingatia masharti yote ya kujikinga na ugonjwa huu.

“Tumeandaa utaratibu mzuri wa kuwahudumia tena wateja wetu na nataka niwahakikishie usalama wao,” alisema.

 Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Fredric Clavier, alisema raia kutoka nchi yake ni miongoni mwa wageni wanaotembelea Zanzibar na wengi wao wanafikia hoteli hiyo.

Alisema zaidi ya watalii 4,500 kutoka Ufaransa hutembelea Zanzibar kwa mwezi hivyo aliuomba uongozi wa hoteli hiyo kusimamia usalama wa wageni.

“Nitaendelea kuwahamashisha wageni hasa kutoka Ufaransa kuendelea kutembelea Tanzania hasa Zanzibar kwa sababu kuna vivutio vingi kwa wageni,” alisema.