LONDON, England
MENEJA wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer, anaonekana kutaka kuendelea na Paul Pogba , baada ya kudhihirisha mahitaji yake kwa kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa.
Kabla ya kuibuka kwa janga la virusi vya ‘corona’ ilikuwa inafahamika kuwa kiungo huyo angeondoka Old Trafford baada ya kuwepo kwa tetesi za kutaka kutimkia Real Madrid au Juventus FC, lakini, sasa anaonekana kufurahia maisha United.
Licha ya tetesi hizo, tangu Pogba arejee uwanjani akitokea kwenye maumivu ya muda mrefu ametengeneza muunganiko mzuri na kiungo mshambuliaji kutoka Ureno, Bruno Fernandes, na kufanikisha uimara wa kikosi cha United.
Mkataba wa Pogba mwenye umri wa miaka 27, utafikia kikomo mwishoni mwa mwaka 2021, lakini uongozi wa klabu hiyo una kipengele cha kumuongezea mkataba mpya.
Endapo Manchester United watafanikiwa kumbakiza Pogba, Solskjaer atakuwa ameingia mkataba na viungo wake wote, ambapo wiki iliyopita alifanikiwa kumsainisha mkataba Mserbia, Nemanja Matic na Scott McTominay.
“Ili kuwa klabu kubwa lazima tuwe na wachezaji wakubwa, tuna matumaini tunaweza kumshawishi kiungo huyo”, alisema, Solskjaer.
“Paul tangu aliporudi kutokea kwenye maumivu anaonekana kuimarika siku hadi siku, anafurahia kucheza nasi, gonja tuone tutakapopelekwa na hili”, aliongeza.
Pogba, ambaye amekuwa akiwindwa kwa muda mrefu na Real Madrid na Juventus, amefunguka kuwa anataka kuendelea kubakia Old Trafford na kwamba, ubora wa kikosi hicho umekuwa ukimpa mzuka zaidi.
Pia, amesema kutua kwa kiungo Bruno Fernandez kumetoa mchango mkubwa kwenye kikosi na anafurahia kucheza sambamba na Mreno huyo.
Kutokana na hilo, Pogba amesema kwa sasa yupo tayari kuanzisha mazungumzo kwa ajili ya mkataba mpya ili kuendelea kukipiga kwa muda mrefu na mashetani wekundu hao.
Pogba mkataba wake wa sasa umebakiza mwaka mmoja kukiwa na kipengele kinachoipa United nafasi ya kumuongezea mwaka mmoja zaidi.
Hata hivyo, imebainika kuwa Pogba aliyenaswa kwa dau la pauni milioni 89 mwaka 2016 anafurahia kucheza sambamba na Bruno ambaye ujio wake umeifanya Man United kuimarika zaidi na kuifanya kupata matokeo mazuri tofauti na mambo yalivyokuwa awali.
Kombinesheni ya Bruno na Pogba imeifanya Man United kuwa moto ikicheza mechi 16 bila ya kupoteza huku ikipiga soka la kuvutia na kuonyesha mwanga wa kurejea kwa kikosi kama kile cha enzi za Sir Alex Ferguson.
Lakini, United watalazimika kumtengea Pogba mshahara mnono zaidi ya anaolipwa sasa wa pauni 290,000
kwa wiki na bonasi nyengine.(BBC Sports).
Pogba ampagawisha Solskjaer
