YERUSALEMU,ISRAEL

POLISI Israeli imetumia maji ya kuwasha kuwatanya waandamanaji waliozingira makaazi ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu kutokana na hasira za madai ya rushwa yanayomkabili kiongozi huyo na jinsi anavyolishughulikia janga la virusi vya corona.

Mjini Jerusalem mamia ya watu walikusanyika nje ya nyumba ya waziri mkuu na kisha kuandamana mitaani kumtaka Netanyahu kujiuzulu wakati polisi ilipotumia maji ya kuwasha kuwatawanya na kuwakamata waandamanaji wawili.

Katika mji wa Tel Aviv, ulio kitovu cha biashara, maelfu ya watu walikusanyika kwenye fukwe kudai msaada wa serikali kwa biashara zilizoathiriwa na janga la COVID-19 pamoja na wafanyakazi waliopoteza ajira au kuwekwa kwenye likizo  bila malipo.

Katika wiki za karibuni raia waisrael wanafanya maandamano karibu kila siku juu ya ukosefu wa ajira, kurejeshwa kwa viuzuizi vya kupambana na virusi vya corona pamoja na tuhuma za rushwa dhidi ya Netanyahu.