NA MWAJUMA JUMA

ZOEZI la uchukuaji fomu za kuwania nafasi za uongozi katika timu ya Polisi Zanzibar linatarajiwa kuanza leo Julai 27.

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Michezo wa Jeshi hilo Kibabu Haji Hassan alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi kuhusu timu yao ambayo inatarajiwa kufanya uchaguzi ifikapo Agosti 9, mwaka huu.

Alisema zoezi hilo litakuwa la wiki moja na litamalizika Agosti 5.

Alieleza timu hiyo inafanya uchaguzi baada ya uongozi uliopo madarakani kumaliza muda wake.

Alitaja nafasi ambazo zitawaniwa katika uchaguzi huo ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu na Msaidizi wake pamoja na mshika fedha na Msaidizi wake.

Alisema viongozi ambao watachaguliwa wataitumikia kwa muda wa miaka minne kama ambavyo katiba ya timu inavyoelekeza.

Awali alisema kabla ya kulikuwa na kazi ya kufanya uhakiki wanachama wao na imemalizika kwa salama na amani.

Alifahamisha kwamba kazi hiyo iliyokuwa ya mwezi mmoja ilikuwa na lengo la kutambua idadi ya wanachama wake na wapiga kura wao.