NA TATU MAKAME

JESHI la Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja limesema litaendelea kufanya operesheni za kupambana na watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya mkoani humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Haji Abdalla Haji, alisema hayo wakati alipozungumza na mwandishi wa habari kufuatia kukamatwa na dawa za kulevya kwa kijana Suleiman Omar Suleiman (30) mkaazi wa Nungwi Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja.

Kamanda Haji alisema tukio hilo lilitokea Julai 21, mwaka huu, majira ya saa 4:30 asubuhi ambapo  mtuhumiwa huyo alipatikana na kete 81 aina ya ‘heroinzen’ zenye uzito wa gramu 1.782 akiwa amezifunga ndani ya pakti ya sigara na kuzihifadhi ndani ya suruwali yake fupi aliyokuwa ameivaa ndani.

Alieleza kuwa kikosi cha jeshi hilo kilifanya opereshen za kupambana na watumiaji,wasambazaji na wauzaji wa dawa za kulevya na kufanikiwa kumkamata.

Hata hivyo, alisema mtuhumiwa atapelekwa mahakamani mara taratibu zitakapokamilika.

Hata hivyo alitoa msisitizo kwa vijana kuacha kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya kwani wanaangamiza nguvu kazi ya taifa.