NA HUSNA SHEHA

JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, limemshikilia John Samwel Manga (32) mkaazi wa Fuoni Migombani kwa kujifanya ofisa usalama wa taifa, ambapo anatumia nafasi hiyo kuwafanyia utapeli wananchi.

Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari juu ya matukio ya wiki yaliyotokea katika mkoa wake Kamanda wa Mkoa huo, Awadhi Juma Haji, alisema kijana huyo alitenda kosa hilo Julai 11 mwaka huu majira ya saa 9:30 jioni huko skuli ya msingi Mnemonic Amani mjini Unguja.

Alisema kijana huyo alipatikana baada ya jeshi hilo kumfuatilia matukio hayo aliyokuwa akiyafanya kwa watu mbali mbali kwa kuwadanganya atawasaidia kuwapa ajira katika Idara ya Usalama wa Taifa na taasisi nyengine za serikali, ambapo alikua akichukua fedha na vitu tofauti.

Alieleza kuwa katika utapeki huo alifanikiwa kumtapeli Asha Omar Hamad kiasi cha shilingi 500,000 ambae alimwambia kuwa atamsaidia kupata ajira katika Idara ya usalama wa Taifa.

Aidha anadaiwa kumtapeli Abubakar Ali Mohammed (24) mkaazi wa Mtopepo kiasi cha shilingi 2,590,000 kopyuta moja aina ya laptop na kamera aina ya canon.

Kamanda huyo alisema kuwa katika uchunguzi wa matukio ya kijana huyo wamefanikiwa kupata nyaraka mbali mbali zikiwemo vyeti vya kumalizia masomo vya watu mbalimbali, vyeti vya kuzaliwa, viapo vya mahakama, kompyuta moja aina ya laptop aina ya Lenovo.

Alisema kuwa vitu vyengine alivyokamatwa navyo ni kamera aina ya canon picha mbali mbali za passport saizi za baadhi ya watu ambao aliwafanyia utapeli huo na bahasha moja ya kaki iliyogongwa muhuri unaosomeka ‘confidential’ na maneno “Director National Security P.O.BOX 2025 DSM”.