NA TATU MAKAME

JESHI la Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, limesema litawachukulia hatua viongozi wa vyama vya siasa watakaotumia lugha za matusi kwenye majukwaa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi Haji Abdalla Haji, alisema hayo Ofisini kwake Mahonda Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja wakati alipozungumza na Gazeti hili.

Alisema wakati wa harakati za kuelekea uchaguzi mkuu imekuwa jambo la kawaida kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kutumia lugha za matusi kwenye majukwaa wakati wanapofanya kampeni dhidi ya viongozi wa serikali wa chama tawala.

Alisema hali hiyo wanaizuiya kwani wamegundua kwamba ni sehemu ya kuvunjika kwa amani hivyo jeshi hilo litahakikisha linafanya wajibu wake wa kisheria dhidi ya watakaokwenda kinyume na sheria za uchaguzi.

“Mtu hakatazwi kufanya kampeni, cha msingi ni kuzingatia wajibu wake wakati anapopanda juu ya jukwaa na kufanya kampeni kwa kutumia lugha za matusi ni kosa kisheria”,alisema.

Alisema kazi ya Jeshi la Polisi ni kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaendelea wakati na kabla ya uchaguzi hivyo jeshi hilo litakuwa makini dhidi ya watu watokwenda kinyume na kuhakikisha linawachukuliwa hatua za kisheria watu watakaoendesha kampeni za matusi majukwaani katika kipindi hicho.