NA HAFSA GOLO
JESHI la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi limesema halitaki kuona vipeperushi vya kisiasa mitaani vyenye kuwachafua wagombea, mikusanyiko wala maandamano kwani kufanya hivyo ni kutasababisha uvunjifu wa amani nchini.
Mrakibu Muandamizi wa jeshi hilo, ambae pia Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Simon Pasua, alieleza hayo wakati alipokua akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Madema mjini Unguja.
Aliwataka wananchi waliokuwa hawakuridhika na matokeo ya kura za maoni majimboni kufuata taratibu na miongozo ya vyama vyao, badala ya kuanzisha maandamano ama vurugu zisizo na tija na hatimae kusababisha machafuko ya kisiasa nchini.
Aidha alivishauri vyama vya siasa kushughulikia malalamiko ya wafuasi wao kwa mujibu wa matakwa ya katiba zao, ili kuhakikisha amani na utulivu inaendelea kudumu nchini hasa katika kipindi hichi kinachoelekea uchaguzi mkuu.