NA HAJI NASSOR, PEMBA
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Ahmed Khamis Makarani, amesema wanaendelea na upelelezi, ili kuwajua waliyohusika na kifo cha kijana Ramadhan Haji Khatib, miaka 34 wa shehia ya Pujini wilaya ya Chake Chake Pemba, kilichotokea Juni 25, mwaka huu.
Alisema, wameunda kikosi kazi cha askari wataalamu, ili kufanya upelelezi huo, na pindi watuhumiwa wa mauwaji hayo wakipatikana, watafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Kamanda huyo alisema, ni vyema wananchi wakawa watulivu katika kipindi hiki wakiendelea na upelelezi, na kubwa kwa sasa, ni kutoa taarifa zozote zitakazosaidia kujulikana kwa watu hao.
Alieleza kuwa, upelelezi wao hauzui kupokae ushauri na taarifa nyingine ambazo zitasaidia kwa njia moja ama nyingine, kufanikisha kukamatwa kwa wathumiwa hao.
“Wananchi waendelee kushirikiana na Jeshi lao la Polisi, maana waliyofanya bila shaka wapo ndani ya jamii, sasa watoe taarifa, ambazo zitasiaidia kwa njia moja ama nyingine kupatikana,’’alieleza. Kamanda huyo wa Polisi mkoa wa Kusini Pemba, Ahmed Khamis Makarani, aliwataka wananchi kuacha utamaduni wa kujichukulia sheria mikononi, pale wanapowakuta watuhumiwa wa makosa mbali mbali.