TEHRAN,IRAN

WAZIRI  wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kurefusha vikwazo vya silaha kwa Iran.

Pompeo alisema Marekani na vikosi vyengine mwezi uliopita waliikamata boti iliyokuwa na silaha za waasi wa Houthi nchini Yemen.

Akizungumza na waandishi habari, Pompeo alisema marufuku ya biashara ya silaha dhidi ya Iran inapaswa kurefushwa ili kuzuia mizozo zaidi katika ukanda huo.

Alisema hakuna mtu yoyote atakayeamini kwamba Iran itazitumia silaha kwa ajili ya malengo ya amani.

Mwanadiplomasia huyo wa Marekani alisema Iran inakiuka marufuku ya silaha dhidi yake, ambayo muda wake unamalizika mwezi Oktoba.

Pompeo alisema silaha zilizokamatwa ni pamoja na maroketi 200, zaidi ya bunduki 1,700, makombora 21 na vifaru kadhaa.