KIGALI,RWANDA
BARAZA la Mawaziri nchini Rwanda limewataka wananchi kuwa makini zaidi katika kuheshimu hatua zilizowekwa za kupunguza kueneza Covid-19 nchini.
“Mkutano wa baraza la mawaziri ulithibitisha hitaji la kuongezeka kwa umakini katika kutekeleza hatua za kuzuia Covid-19 na kutoa wito kwa umma kupunguza harakati zisizo za lazima ikiwa ni pamoja na kutembelea marafiki na familia,”ilieleza taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.
Azimio hilo linatokana na maonyo ya hivi karibuni yaliyotolewa na Polisi wa Kitaifa wa Rwanda (RNP), juu ya kutofanya hafla za nyumbani na mikusanyiko mingine isiyo ya lazima ambayo yanaweza kusababisha kuenea kwa maambukizo ya Covid-19.
Mkutano wa baraza la mawaziri pia uliamua kwamba mikusanyiko ya watu katika maeneo ya umma na nyumbani ni marufuku, na kuongeza kuwa mahudhurio ya shughuli za pamoja yasizidi watu 15 kwa wakati mmoja.
Pia, maeneo ya ibada,yanaweza kuanza tena kutoa huduma lakini kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa na Wizara ya Serikali za Mitaa ambapo pia skuli,baa na vilabu vya usiku vitaendelea kufungwa.
Hadi sasa Rwanda iliripoti kesi 37 mpya za Covid-19 na 31 waliopona.
Kati ya kesi hizo mpya, kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Afya, 15 waligunduliwa katika maeneo hatarishi ya wilaya ya Rusizi.
Pia, kesi 13 za Covid-19 zilirikodiwa Kigali kwa wakaazi ambao walikuwa wametengwa walipofika.
Wakati huo huo, wilaya za Nyamasheke na Rulindo pia zilithibitisha kesi sita mpya za Covid-19 .
Tangu kuzuka kwa janga hili nchini katikati mwa Machi, nchi imeongeza vitendea kazi vya upimaji wa Covid-19, ambapo nchi hadi sasa imefanya jumla ya vipimo vya sampuli 255,959 .