Rais mstaafu wa serikali ya awamu ya tatu nchini Tanzania Benjamin William Mkapa amefariki akiwa na miaka 81.

Rais John Pombe Magufuli ametangaza usiku wa kuamkia leo Ijumaa kupitia runinga ya taifa taarifa za kufariki dunia kwa kiongozi huyo wa awamu ya tatu katika hospitali moja jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa matibabu.

“Nimesikitishwa na kifo cha Mzee wetu Benjamin Mkapa (Rais Mstaafu wa Awamu ya 3), nitamkumbuka kwa mapenzi yake makubwa kwa Taifa, ucha Mungu,uchapakazi na utendaji wake katika kujenga uchumi, hakika Taifa limepoteza nguzo imara, Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, Amina”-

Taarifa zaidi juu ya msiba huo na mipango ya mazishi zinatarajiwa kutolewa baadae hii leo.

Mzee Mkapa alizaliwa Novemba 1938, Mkoani Mtwara kusini mwa Tanzania, na aliliongoza taifa hilo kwa mihula miwili toka mwaka 1995 mpaka 2005.