GITEGA,BURUNDI

RAIS  mpya wa Burundi Evariste Ndayishimiye ametakiwa kulipa kipaumbele suala la kuchunga na kutetea haki za binadamu katika utawala wake baada ya serikali ya kabla yake kuandamwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu.

Hayo yalielezwa na  Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch kwa Rais huyo ambapo lilipendekeza mambo manane ambayo yataweza kuboresha hali ya haki za binadamu nchini humo katika mwaka wa kwanza wa uongozi wake.

Moja ya mapendekezo hayo ni kuwafuta kazi maofisa usalama wote wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ukandamizaji dhidi ya raia sambamba na kuleta mageuzi ya kidemorasia katika nchi hiyo.

Jenerali Mstaafu Evariste Ndayishimiye alichukua hatamu za kuiongoza Burundi baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi uliofanyika Mei 20 mwaka huu.

Serikali ya Burundi chini ya uongozi wa Nkurunziza iliandamwa na tuhuma nyingi za  kufanya ukandamizaji mkubwa wa umwagaji wa damu dhidi ya wapinzani katika kona mbalimbali za Burundi.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanalituhumu moja kwa moja tawi la vijana la chama tawala cha CNDD-FDD kuwa ndio wanaohusika na mauaji ya wapinzani.

Hata hivyo serikali ya Burundi imekuwa ikikanusha madai hayo na kueleza kwamba, ni propaganda chafu dhidi ya serikali ya nchi hiyo ambazo zimekuwa zikiendeshwa kwa kutegemea vyanzo visivyo vya kuaminika.