NA NASRA MANZI

MKUU wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed Mahamoud amesema sherehe za kijadi za mwaka kogwa zitaongeza thamani na kuwa chachu ya kuongeza uchumi wan chi.

Akizindua sherehe hizo huko Kae Kuu Makunduchi, Ayoub alisema kuwepo kwa tamasha hilo kutaongeza pia nguvu ya kuja kwa wageni na kupatikana kwa pato nchini.

Mkuu huyo alisema si vyema kuacha mila, desturi na utamaduni kwa kufuata maneno ambayo hayaleti tija katika jamii kwa lengo la kupotosha tamaduni.

Alisema kila nchi inajivunia na kuona fahari utamaduni wake na kwamba tamasha hilo la jadi linapaswa kuendelezwa.

“Nimefarajika kuona katika sherehe hizi ngoma za asili kwani zinasaidia thamani ya kuwavuta wageni kwa kusherehesha mwaka kogwa, tuendelezeni tamaduni kwa kujenga taifa letu”, alisema.

Aidha alitaka kamati ya wazee inayoshughulikia mwaka kogwa kufanya maandiko kwa ajili ya kumbukumbu za kujua historia kwani itawapa fursa kwa wageni wanaofika kwa ajili ya kushuhudia sherehe hizo.

Pia alisema sherehe za mwaka kogwa zimefana kutokana na mwamko wa watu na kuonesha umoja na mshikamano wa kufanikisha na kuunga mkono wenzao kutoka sehemu tofauti ili kuendeleza utamaduni huo.

Alipongeza kamati ya mwaka kogwa kwa jitihada wanazozichukua katika kufanikisha utamaduni, jambo ambalo litawainua vijana katika kujipatia fursa pale wageni wanapowasili na kujua utamaduni huo.

Nae mkuu wa Wilaya ya Kusini, Idrisa Mustafa kitwana alisema ni vyema kuendelea kuimarisha zaidi utamaduni huo wa mwaka kogwa ili kuongezeka kwa wageni nakutangaza utamaduni uliopo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Mwaka Kogwa Mwita Masemo alisema hawanabudi wananchi wa Makunduchi kuendeleza mila na utamaduni wao.

Alisema si vyema baadhi ya watu kubeza tamaduni ambazo zinaleta mafanikio katika jamii, jambo ambalo litakua na kuongeza nguvu kwa vizazi vya sasa na baadae kuinua utamaduni huo wa sherehe za kijadi.