NA MARYAM HASSAN

ALIYEDAIWA kumtorosha msichana wa miaka 17 kutoka skuli ya Nyerere na kumpeleka nyumbani kwao huko huko Nyerere, amenyimwa dhamana na mahakama ya mkoa Vuga.

Mshitakiwa huyo ni Hamza Alawi Pandu (19) mkaazi wa Nyerere, indaiwa kuwa baada ya kumtorosha msichana huyo alimbaka, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Kijana huyo aliiomba mahakama impe dhamana chini ya Hakimu Hussein Makame, juu ya shitaka linalomkabili mshitakiwa huyo.

Hamza alifikishwa mahakamani kwa makosa mawili  ikiwepo kosa la kubaka na kutorosha, ambapo kwa kosa la kubaka halina dhamana na kutorosha linadhaminika.

Akisoma hati ya mashitaka kwa mshitakiwa huyo, wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Simni Mohammed alisema.

Mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Juni 8 mwaka jana majira ya saa 4:30 za asubuhi huko Nyerere wilaya ya Mjini Unguja.

Mshitakiwa alimuingilia msichana wa miaka 17 na kabla ya kutenda kitendo hicho, anadaiwa kumtorosha kutoka skuli ya Nyerere na kumpekeka nyumnani kwao huko huko Nyerere, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Baada ya kusomewa maelezo hayo, Hakimu Hussein aliahirisha shauri hilo hadi Agosti 3 mwaka huu, kesi yake itakapo anza kusikilizwa ushahidi kwa kuwa upande wa mashitaka umeeleza kuwa upalelezi umekamilika.