KIGALI,RWANDA

MAENEO ya ibada yameruhusiwa tena kufungua shughuli zao baada ya kufungwa zaidi ya miezi nne, ili kupambana  na janga la Covid-19 lililoikumba dunia.

Uamuzi wa kufungua maeneo ya ibada ulitolewa baada ya mkutano wa baraza la mawaziri uliosisitiza kwamba shughuli zote zitarejea katika hali ya kawaida baada ya ukaguzi ili kuhakikisha wanakidhi vizuizi vilivyowekwa.

Katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ilibainika kuwa Wizara ya Serikali za Mitaa itatoa miongozo inayoweza kuzingatiwa na maeneo ya ibada katika suala hilo.

Bodi ya Utawala ya Rwanda (RGB)  ilitoa mwongozo  wa kufuatwa katika maeneo ya ibada kabla ya kuruhusiwa kufunguliwa tena.

RGB pia ilisisitiza kwamba kila nyumba ya ibada lazima iwe na wasafishaji wa mikono, vipimo vya joto pamoja na barakoa.

Pia,katika tukio la kufungua tena maeneo hayo alisema RGB, watoto chini ya miaka 13 hawatoruhusiwa kuhudhuria,wakati wale walio na umri wa miaka 13 hadi 18 watahudhuria kwa kushirikiana na mzazi au mlezi.

Kwenye barua hiyo, Baraza la Kidini lilipewa jukumu na RGB kuchagua nyumba za kufanyia ibada zinazofikia na kukidhi kiwango cha usalama.

Nchi hiyo iliripoti kesi 19 mpya na waliopona 15, na hivyo kufanya idadi ya kesi zilizothibitishwa kuwa 1,435.

Rwanda tangu katikati ya Machi, wakati  kesi ya kwanza ya Covid-19  iliripotiwa, ilifanya vipimo vya sampuli 194,802 na iliripoti vifo vinne kutokana na janga hilo.