MUNICH, Ujerumani

HATIMAYE klabu ya Bayern Munich na bingwa wa ligi ya Bundesliga imemtambulisha Leroy Sane ambaye amesema kwamba amehamia kwenye klabu hiyo, ili kuchukua ubingwa wa michuano mikubwa ya Ulaya. Sane anatokea klabu ya Manchester City ya England.

“Kama nikihama, maana yake ninahamia kwenye klabu inayoshinda michuano ya klabu bingwa Ulaya, na Bayern inaweza kushinda, kwa asilimia 100,” alisema Sane. Mchezaji huo wa miaka 24 aliongeza kuwa anataka kuwa “kivutio kipya”.

Sane hata hivyo hataweza kucheza katika michuano ya klabu ya bingwa ya msimu wa 2019/20 wakati itakaporejea mwezi Agosti kwa kuwa hajasajiliwa.

Amesema, kikosi cha Bayern cha sasa ni cha”kiwango cha juu”, chini ya kocha wake Hansi Flick, aliyekibadilisha vizuri sana tangu alipoteuliwa Novemba 2019.

Sane aliyenunuliwa kwa kitita cha dola milioni 58 kutoka City alitakiwa kuchagua jezi ya kati ya namba ya Saba na 10. “Nilichagua namba 10 kwa sababu ninataka kuongoza”, amesema mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani.