MUNICH, Ujerumani

ANDRE SCHURRLE  aliyeisaidia timu ya taifa ya Ujerumani kunyakua kombe la dunia 2014, ameamua kutundika madaluga juu akiwa tu  na umri wa miaka 29.

Schurrle ambaye aliruhusiwa kuondoka Borussia Dortmund siku ya Jumatano, ameamua kutundika daluga baada ya kushindwa kurudia ubora wake wakati akiichezea Bayer Leverkusen na Chelsea.

Ameliambia gazeti la Der Spiegel, “Sihitaji tena kupigiwa makofi.”

Mshambuliaji huyo alikuwa miongoni mwa kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani kilichoshinda kombe la dunia mwaka 2014 huku akifunga mabao mawili katika mechi ya nusu fainali dhidi ya Brazil wakati Ujerumani ilipoiadhibu Brazil 7-1.

Alijiunga na Chelsea mwaka 2013 baada ya kupata mafanikio akiwa na klabu yake ya Leverkusen, kisha baadaye akarudi tena Bundesliga na kuichezea Wolfsburg mwaka 2015.

Andre Schurrle akiwa na timu yake ya mwisho aliyopelekwa kwa mkopo na Borussia Dortmund, Spartak Moscow

Schurrle alijiunga na Dortmund mwaka 2016 lakini akashindwa kufikia makali yake akiwa Signal Iduna Park, kabla ya kuondoka na kuzichezea kwa mkopo Fulham na Spartak Moscow.

Mara ya mwisho kuichezea Dortmund ilikuwa mwaka 2018, lakini pande zote mbili zimekubaliana kwa hiari kumaliza mkataba wake uliostahili kukamilika mwaka ujao.