NA HUSNA MOHAMMED

LICHA ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuweka biashara huria, lakini baadhi ya watu wamekuwa wakitumia vibaya fursa hiyo jambo ambalo linakwenda kinyume kabisa na azma ya Serikali.

Fursa kama za uwekezaji katika sekta ya afya, uwekezaji wa mahoteli na nyumba za kulala wageni, sekta ya elimu na mengi mengineyo kwa kiasi kikubwa huwahusisha wazawa na hata wageni.

Nasema hivyo kwa sababu mambo haya yanategemeana kwa kuwa kila mahala panahitaji uzoefu na taaluma ya kazi husika.

Kwa mfano sekta ya afya ni lazima kupata wataalamu wa vitengo mbalimbali vya afya ya binaadamu, sekta ya elimu kupata wataalamu wa masomo mbalimbali ikiwemo ya Sanaa na ya sayansi na sehemu za mahoteli kupata wapishi wa vyakula vya ndani na vya kigeni na kazi nyengine zinazohitajika katika eneo hilo.

Ni hapo juzi tu gazeti hili lilitoa taarifa inayohusiana na ‘Kupigwa marufuku nyumba za makaazi kutumika skuli’ sambamba na ‘Leseni za walimu wasio na sifa kusitishwa’.

Kwa kweli taaswira hizi mbili za habari zinaleta sura mbaya kwa kuwa elimu ni jambo la kwanza linalosababisha kuwapata wataalamu wa fani zote zinazojulikana.

Ni ukweli usiopingika kuwa bila ya elimu basi hivi sasa kusengekuwa na wataalamu wa fani mbalimbali, hivyo elimu inapoanza kubezwa hapa mwanzo ni vipi wataalamu wa fani hizi wanaweza kupatikana?.

Leo hii kuna baadhi ya watu wamekuwa wakifungua skuli kwenye nyumba wanazoishi ni jambo la kushangaza na linalohitaji kuchukuliwa hatua ya kipekee ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria kwa wahusika.

Imetajwa katika taarifa hiyo kuwa pamoja na nyumba kutumika kama skuli lakini vyombo vya madarasa havikidhi kabisa uchukuaji wa wanafunzi kwa mukhtaza wa kimazingira ya usalama kwa watoto wanaokusudiwa kusoma.