KIGALI,RWANDA

UHABA wa walimu waliohitimu imeilazimisha serikali kuendelea kuajiri waliofaulu digrii ambao hawakuendelea masomo ili kujaza nafasi zilizo wazi.

Akizungumza na vyombo vya habari,Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya elimu ya Rwanda (REB) Angelique Tusiime alisema kuwa kuajiri walimu wasio na sifa kunachochewa na pengo kubwa liliopo la idadi ya walimu wanaozalishwa na vyuo vya Mafunzo ya Ualimu na vyuo vikuu na kuangalia ni kitu gani kinachohitajika skuli.

Mjadala wa kuwaondoa na kuwaweka waendelee wasio na sifa za uwalimu umekuwa ukiendelea tangu mwaka 2016.

Hadi kufikia Oktoba 2019, Wizara ilikuwa inatoa uamuzi ambao utawaona walimu wasio na sifa  wakiondolewa kwa majukumu yao katika miezi miwili .

Tusiime alisema kumekuwa na changamoto katika kupata idadi ya waalimu kujaza mapengo akibainisha kuwa mnamo mwaka wa 2019, ni walimu 3000 tu kwa skuli za maandalizi na msingi waliyohitimu TTC na vyuo vikuu.

Alisema hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba ni asilimia kumi tu ya walimu waliopata mafunzo ndio waliochaguliwa kufanya kazi katika skuli mbali mbali nchini.

Hadi mwaka huu, kulikuwa na nafasi 3,000 za wazi katika skuli za msingi lakini Tusiime alisema idadi hiyo imepanda.

Alisema  Serikali inaongeza idadi ya vyumba vya madarasa, lakini walimu wengine wanastaafu hali ambayo imesababisha idadi ya walimu ambao wanahitajika kuongezeka hadi kufikia 7,000.