NA KAUTHAR ABDALLA

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza kuwa inaendelea kuandaa mipango ya muda mfupi na mrefu inayolenga kuimarisha uchumi na kuondoa umasikini nchini.

Utekelezaji wa mipango hiyo, uliongeza umuhimu wa mahitaji ya takwimu bora kwa ajili ya kufuatilia, kutathmini na kupima mafanikio yatakayopatikana.

Hayo yalielezwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Dk. Makame Ali Ussi, alipokuwa akifungua mafunzo ya wadadisi wa sensa ya kilimo na mifugo kwa mwaka wa kilimo 2019/20 yaliyofanyika katika jengo la ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya mapinduzi Zanzibar, Mazizini.

Alisema miongoni mwa mipango na programu hizo ni kuendeleza sekta ya kilimo (ZASDP), mpango wa utayarishaji wa dira mpya ya maendeleo ya Zanzibar 2050 na mpango wa kutayarisha mpango mkakati wa muda wa kati wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini Zanzibar.

Alisema sensa ni muhimu kwani itasaidia kupatikana takwimu za viashiria mbalimbali ambavyo hutumika katika kutathmini utekelezaji wake.

“Lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha washiriki kufahamu taratibu zote zinazohusiana na kazi ya kudadisi katika sensa hiyo ambayo ni muhimu katika kusaidia kupatikana takwimu za viashiria mbalimbali ambavyo hutumika katika kutathmini utekelezaji wa shughuli za serikali katika sekta ya kilimo,” alieleza Dk. Ussi.

Aidha alieleza kuwa takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2019, mchango wa sekta ya kilimo katika pato la taifa ulikuwa asilimia 21.2 kati ya asilimia hiyo, kilimo cha mazao kilichangia asilimia 7.4, mifugo asilimia 7.8, misitu asilimia 1.2 na sekta ya uvuvi asilimia 4.8.

Alisema takwimu za mwaka 2019 zilionyesha kuwa jumla ya ekari 29,975.7 zilipandwa mpunga, ekari 30,204.3 zilipandwa muhogo, ekari 7,595.5 zilipandwa migomba na zaidi ya ekari 10,000 zilipandwa mazao ya mboga mboga.

Alifahamisha kuwa pamoja na uwepo wa takwimu hizo, taarifa zinaonyesha kuwa bado kuna mahitaji makubwa ya takwimu katika mipango ya maendeleo ya kitaifa.