NA KHAMISUU ABDALLAH

SERIKALI ya Mapinduizi Zanzibar imesema imeridhishwa na hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa barabara zote zilizokusudiwa kukamilika katika awamu ya saba.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Mohamed Ahmada Salum, aliyasema hayo alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa barabara za Mkoa Mjini.

Alisema, hatua hiyo imeweza kuipa matuamaini makubwa serikali katika kuona inawapatia maendeleo ya kijamii wananchi wake.

Aidha alisema, serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili kuimarisha miundombinu ikiwemo barabara, ili kuhakikisha wananchi wanafanya shughuli zao za kimaendeleo bila ya matatizo yoyote.

Hivyo, aliwasisitiza wakanadarasi kuhakikisha wanamaliza kazi kwa wakati uliopangwa, ili kuepusha gharama zitazoweza kujitokeza kutokana na uchelewaji wa ujenzi huo.

Nae, Mshauri Elekezi wa Kampuni ya CCECC Nekodemas Sikambale, alisema ujenzi wa barabara hizo umefikia asilimia 70 hadi sasa na wanatarajia kumaliza mwishoni mwa mwezi huu.

Aidha, alisema ujenzi wa barabara ya Kwanyanya hadi Polisi ulikwama kutokana na kujenga daraja ambalo halikuwepo katika mkataba wa ujenzi.