KABUL,AFGHANISTAN
SHAMBULIZI la angani lililofanywa na serikali ya Afghanistan limesababisha vifo vya watu 14 katika mkoa wa Herat Kaskazini mwa nchi hiyo wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Kwa mujibu wa aliyeshuhudia tukio hilo Noor Rahmati aliyepoteza jamaa zake watatu katika shambulizi hilo, mamia ya watu walikuwa wamekusanyika katika eneo la Adraskan mkoani humo kumkaribisha nyumbani aliyekuwa mpiganaji wa kundi la Taliban Ghulam Nabi aliyeachiwa huru kutoka jela wakati shambulizi hilo lilipotokea.
Maofisa wa serikali walisema jana kuwa shambulizi hilo lililofanywa linachunguzwa.
Nabi alikuwa ameachiwa huru katika mpango wa kubadilishana wafungwa unaolenga kusogeza mbele mazungumzo ya ndani ya serikali ya Afghanistan na kundi la Taliban hii ikiwa ni awamu ya pili na muhimu ya mkataba wa amani kati ya Marekani na Taliban. Katika ujumbe kupitia ukurasa wa twitter, mjumbe wa amani wa Marekani katika mazungumzo hayo Zalmay Khalilzad alishtumu ghasia hizo na kupongeza hatua ya serikali ya kufanya uchunguzi.