NA MWANDISHI WETU

SIMBA imeibuka na ushindi wa mabao 5-1 mbele ya Alliance FC kwenye mchezo wa ligi kuu Bara uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ambao ulikuwa mkali na kupendeza kwa muda wote, huku Simba ikishusha nyota wake wengi, tofuati na mchezo dhidi ya Mbao ambapo ilifungwa mabao 3-2.

 Alliance FC ilianza mchezo kwa kulishambulia lango la Simba ili kutafuta bao la mapema, lakini uimara wa walinzi wa timu hiyo waliweza kuzuwia hatari ambazo zilielekezwa kwao.

Hata hivyo Simba nao walijipanga na kujibu mashambulizi hayo ambapo walipata majibu katika dakika ya dakika 24, kwa kuanza kuandika bao la kwanza lililofungwa na Meddie Kagere kwa penalti.

Baada ya bao hilo Alliance FC walikuja juu na kujibu mashambulizi hayo wakitafuta bao la kusawazisha, juhudi hizo zilifanikiwa dakika ya 38 likifungwa na Martin Kigi, ambayo yalidumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.

Kipindi cha pili Simba ilianza kwa kuliandama lango la wapinzani wao na kupata bao la pili  dakika ya 63 likifungwa tena na Meddie Kagere.

Simba iliendelea kujenga maskani langoni mwa wapinzani wake kutafuta mabao zaidi na kiungo Luis Miqussone alifunga bao la tatu dakika  63.

Jahazi la Alliance FC liliendelea kuzama katika dakika ya 66 baada ya  Deo Kanda kuandika bao la nne, wakati karamu ya mabao ilihitimishwa na kiungo Said Ndemla kwa kufunga bao la tano dakika ya 87.