NA MWANTANGA AME

SERIKALI ya Zanzibar hivi sasa imekamilisha upatikanaji wa bajeti yake ya serikali ambayo imepanga kutumia shilingi trilioni 1.4 ambazo zitatumika kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

Kupitishwa kwa Bajeti hii itaweza kutumika kwa ajili ya kufanyia shughuli nyingi katika mipango ya serikali ikiwa ni hatua itayoifanya Zanzibar kupata maendeleo.

Matumizi ya Shilingi Trilioni 1,579.2 kwa mwaka huo wa fedha wa 2020/2021. Kati ya matumizi hayo, shilingi bilioni 969.3 ni kwa ajili ya kazi za kawaida na shilingi bilioni 609.9 kwa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo.

Hii ni kutokana na bajeti hiyo kuweka miradi mbali mbali ya kimendeleo inayokusudiwa kutekelezwa kwa mwaka huo wa fedha ambapo juzi tuu umeanza rasmi matumizi yake.

Kuanza kwa matumizi ya bajeti hiyo tayari imeanza kuwapa matumaini wananchi kwamba yale waliyokuwa wakiyatarajia basi yatakuwa ndani ya kipindi kifupi na kirefu.

Baadhi ya mambo hayo ni kwamba serikali imepanga kutekeleza miradi inayohusu jamii moja kwa moja, na ipo ile itayohusu faida yake kwa serikali.

Moja ya jambo ambalo limekuwa likizungumza sana na serikali katika mijadala mingi iliyojitokeza wakati wa kuipitisha bajeti hii ndani ya kikao cha Baraza la Wawakilishi ni suala la ulipaji wa fidia ulikuwa ukihushisha mambo mbali mbali.

Hili lilionekana kujitokeza katika miradi mingi inayosimamiwa na serikali hasa ile mikubwa kama vile jengo la Terminal III katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume, Ujenzi wa Barabara Kisiwani Pemba, na maeneo yaliopitiwa na Utafiti wa Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia.

Wananchi wanaoishi katika maeneo hayo wamekuwa wakidai kulipwa fidia ikiwa ni hatua wanayoitaka serikali yao iwatimizie ili waweze kutimiza malengo yao.

Ingawa hili ni haki yao, lakini inaonekana hivi sasa suala hili linafanyika kama kuikomoa serikali kwani baadhi yao wamekuwa wakiona kwamba fidia yao ifanane na vile wanavyotaka wao.

Hili ni kutokana na kujionesha baadhi ya watu wamekuwa wakipeleka makisio makubwa ya kudai fidia yao serikali, jambo ambalo linakuwa haliendani na thamani ya mali yake.

Mfano halisi wapo ambao wamepisha maeneo yao kwa ajili ya kupisha barabara mpya, ambapo amevunjiwa nyumba yake ambayo ni ya udogo au ya miti, lakini ipo barabarani basi anadai malipo yanayopindukia ujenzi wa nyumba mpya ya tofali tena ya ghorofa na eneo kubwa lililomzunguka.

Hali hiyo, imeifanya serikali kuwa na wakati mgumu wa kuweza kumudu gharama hizo, kwa vile tathimini iliyofanywa kuonekana hailingani na thamani nyumba iliyovunjwa, kwa vile imeonekana baadhi yao wameamua kupisha ili kutimiza malengo na sio kama wameridhika.

Kutokana na hali hiyo ni wazi kwamba hivi sasa serikali inapaswa kuandaa utaratibu mpya utaoifanya ibaki salama  na kutimiza malengo yake, ili iepukane na lawama za kuchukua muda mrefu wa ulipaji fidia.

Nasema hivi kutokana na kuwa wanaopisha miradi ya serikali wengi wao watakuwa wanahitaji sehemu mpya ya kuanzisha maisha yao, basi iwe inawapa fursa ya kuchagua maeneo ama kutumia zile sehemu ambazo zimechagua kuwagaiya wananchi.

Maeneo hayo yakishakupatikana basi serikali nafikiri ndio iyatumie kuanzisha ujenzi wa nyumba kwa fedha zake, ambayo itakuwa ni ya fidia ya mtu yoyote anaevunjiwa pahala pake, ili  isaidie kupunguza gharama kwani ujenzi huo utazingatia vigezo vyote kwa gharama halisi na sio mtu anavyojipangia.

Hili ni lazima lizingatiwe kutokana na kwamba hali hivi sasa hairidhishi, kwani wapo ambao wanaona kama kupisha miradi ya maendeleo ni fursa ya utajirisho, kwani wamekuwa wakidai viwango vikubwa vya fedha wanazotaka walipwe.

Vile vile, inawezekana hilo likawa linafanyika kwa vile baadhi ya watendaji wanaopewa kazi ya kufanya tathmini wapo ambao sio waaminifu, kwani wanaweza wakawatumia watu hao kupandikiza kudai fedha nyingi na kisha kumbe chao kimo humo humo, jambo ambalo linahitaji kuangaliwa.

Hili linahitaji kuangaliwa kutokana na kuwa bado serikali inahitaji kutumia sehemu nyingi kwa ajili ya kupisha maendeleo, jambo ambalo wasipoliangalia linaweza kuwaweka katika wakati mgumu kufanikisha mipango yao kwani thamani ya eneo inaongezeka mwaka hadi mwaka.

Hivyo basi, ipo haja kufanya aina ya mabadiliko ya ulipaji wa fidia kwa kufikiria wale wote ambao watakumbana na kadhiya hiyo, basi wapatiwe msaada wa kujengewa nyumba kabisa na serikali, badala ya kuwaachia kuweka thamani wanazotaka.

Hili litasaidia kwa kiasi kikubwa kwa serikali kupunguza gharama za ujenzi wa nyumba hizo, na vile vile kuwa na maeneo stahiki yanayoteuliwa kwani zitakuwa katika sehemu zisizoiletea athari ya baadae ikikubwa na mafuriko ama majanga ya aina yoyote.

Inasikitisha sana kuona hivi sasa kuna baadhi ya wananchi nyumba zao zilishatiwa thamani ya kufidiwa, lakini ubomoaji wake unakuwa ni upande mmoja tuu kisha mtu anaachwa achukue eneo jengine hapo hapo ajenge ama kujisogeza tuu.

Naandika hili si kwamba wanachi wasiruhusiwe kudai fidia, laaa hasha ila mtazamo wangu ni kwamba serikali isipojipanga na hili huko mbele itajikuta ikiwa na mzigo mkubwa wa madeni ya wananchi yanayotokana na fidia, jambo ambalo linaweza kuifanya kuonekana haijali kero zao.

Hivyo basi, ipo haja, ikauona mpango huu, ili uisaidie kuondosha lawama kwani ‘Nchi hujengwa na wananchi wenyewe’.