NA NASRA MANZI
WAZIRI wa Fedha na Mipango Zanzibar Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa amesema Serikali itahakikisha inaendeleza ujenzi wa miradi ya kimaendeleo katika maeneo tofauti ya mji wa Zanzibar ili kukuza uchumi wa nchi .
Akizungumza katika ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo iliyopo eneo la Kwahani na Kisonge alisema katika kufanikisha hilo Serikali inatayajia kujenga mji mpya katika shehia ya Chumbuni, Miembeni na Vikokotoni, ili wananchi waweze kupata makaazi bora.
Pia alisema lengo la Serikali kuhakikisha Zanzibar inakuwa na majengo ya kisasa na yenye kuvutia pamoja na Serikali kuongeza vitega uchumi.
Hata hivyo, Waziri Ramia alitembelea miradi ya maendeleo iliyopo kisonge na kuwataka wakandarasi wa ujenzi huo kuhakikisha miradi hiyo inamalizika kwa wakati kabla ya kumalizika kwa awamu ya saba.
“Tumepiga hatua na awamu ya saba imefanya kazi kubwa katika miradi yetu ni vyema kumalizika kwa wakati awamu zijazo kuiendeleza “ alisema
Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini Mfuko wa ZSSF, Suleiman Rashid Mohamed alisema miradi hiyo itasaidia katika maeneo yatakayotumika kuongezeka kwa uchumi na kupata maendeleo.
Mshauri Elekezi wa Kampuni ya ujenzi wa nyumba za maendeleo ya mji mpya wa Kwahani Adrian Eradius, alisema miongoni mwa matatizo yanayowakabili katika kutekeleza mradi kutofika kwa baadhi ya vifaa walivyoagiza kutokana na kuwepo kwa maradhi ya corona.