MOGADISHU,SOMALIA
SOMALIA imeipongeza Uturuki kwa hatua yake ya kufungua tena Msikiti wa Hagia Sophia baada ya miaka 86.
Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kidini Somalia,ilisema inaupongeza umma mzima wa Waislamu na hasa Taifa la Uturuki kwa kuchukua uamuzi wa kurejesha hadhi ya Hagia Sophia kuwa msikiti.
Sherehe kadhaa zilifanyika katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu kusherehekea kufunguliwa tena Msikiti wa Hagia Sophia.
Swala ya kwanza ya Ijumaa ilisaliwa Ijumaa iliyopita katika msitiki wa Hagia Sophia nchini Uturuki tarehe 24 mwezi huu baada ya miaka 86 kwa kuhudhuriwa na Rais, viongozi wa serikali na pia wananchi wa nchi hiyo.
Swala hiyo ya Ijumaa ilifanyika wiki mbili baada ya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan kutangaza kwamba,jengo hilo lenye umri wa karibu miaka 1,500 litafunguliwa kwa ajili ya ibada ya Waislamu kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu wa ubadilishaji matumizi ya jengo hilo lililofanywa jumba la makumbusho na mwanzilishi wa Uturuki ya sasa mwanzoni mwa miaka ya 1930.
Jengo hilo la Hagia Sophia lilijengwa mwaka 537 Miladia (CE) na lilipata umaarufu kutokana na ukubwa wake na wakati huo lilikuwa jengo kubwa zaidi duniani.