NA ABOUD MAHMOUD

WANAFUNZI nchini wametakiwa kuitumia wiki ya elimu ya juu kupata taarifa na kuchagua vyuo sahihi vya kujiunga navyo ili kuepuka kujiunga na vyuo visivyotambuliwa.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma, alieleza hayo wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya elimu ya juu Zanzibar katika mnara wa kumbukumbu ya mapinduzi Michenzani Mwembe Kisonge, Unguja.

Waziri huyo alisema kumekuwa na wimbi la vyuo visivyokidhi vigezo ndani na nje ya nchi na kuwafanya wanafunzi wanaojiunga kupata hasara baada ya kutambua kwamba havistahiki.

“Wito wangu kwenu kutumia maonyesho haya ya wiki ya elimu ya juu katika kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo kutambua vyuo ‘feki’ na ili kupunguza hasara na usumbufu mara baada ya kumaliza masomo,” alisema.

Waziri Pembe alisema kuwepo kwa maonyesho hayo yatamsaidia mwanafunzi katika mambo mbali mbali ikiwemo kutumia fursa ya kuchagua vyuo pamoja na masomo wanayoyataka.

Aidha alisema uwepo wa maonyesho hayo utasaidia walengwa hao kujifunza namna gani ya kuomba na kupata mkopo ambao utawasaidia katika malipo na matumizi wakati wakiwa vyuoni.

“Maonyesho haya yana faida sana kwa vijana wetu ambao wanataka kuendelea na elimu ya juu hivyo ni vyema wakaja hapa kujifunza mambo ambayo yatawasaidia ikiwemo kupata fursa ya udhamini, kuchagua masomo wanayoyataka na jinsi ya kupata mkopo,” alifafanua waziri Pembe.

Alisema vyuo vikuu vyote vina fursa za kutangaza elimu wanazozitoa kuanzia ngazi ya stashahada hadi kufikia uzamivu ili wanafunzi waone umuhimu wa kuvichagua.

Pia aliwataka waandaaji wa maonyesho hayo kuhakikisha yanakuwa endelevu kwa kila mwaka kufanyika ili wanafunzi wapate kujifunza kupitia hapo.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Charles Kihampa, alisema fursa iliyotolewa ya kufanyika maonyesho hayo ni chache sana na si aghlabu kufanyika hivyo ni vyema wanafunzi wakatumia vyema fursa hiyo kutanua ufahamu wao kwa elimu ya juu.