NA MWANDISHI WETU SHINYANGA
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack amekabidhi kiasi cha Shilingi Milioni 42.3 zilizorejeshwa na TAKUKURU Mkoani Shinyanga.
Fedha hizo ni mali ya wastaafu watano ambao awali walikopa kwa nyakati tofauti kwa watu binafsi, wenye biashara ya ukopeshaji fedha binafsi na kuwataka wastaafu kote nchini kukopa katika Taasisi za fedha zinazotambulika kisheria.
Fedha hizo ni sehemu ya kiasi cha shilingi milioni 110.7 ambazo wakopeshaji hao, wanatakiwa kurejesha na Mkuu wa Mkoa amewataka TAKUKURU kuhakikisha fedha zinazodaiwa zinarejeshwa kwa wakati, kwa lengo la kuhakikisha haki ya wastaafu hao inatendeka na kuwataka wastaafu hao kuweka fedha zao Benki ili kuepuka kutapeliwa tena.
Telack pia amewataka TAKUKURU Mkoani Shinyanga kuhakikisha wahusika wote walioshiriki kutapeli fedha ya wasataafu hao, wanafikishwa katika vyombo vya dola na kumuagiza Kamanda wa Jeshi la Polisi Shinyanga kushirikiana na TAKUKURU kutekeleza agizo hilo.
‘’Hawa ni Wastaafu tayari wameitumikia serikali, nawashangaa vijana ambao wanawaibia wazee wenye zaidi ya miaka 60, jambo hili halikubaliki pamoja na kwamba wamerejesha fedha hizi wachukuliwe hatua za sheria, ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaofanya kazi hizi kwa lengo la kutapeli.’’Alisema.
‘’Mteja anakopa kiasi cha shilingi Milioni 2 lakini katika nakala ya mkataba anaobaki nao mfanyabiashara anaongeza tarakimu ili isomeke milioni 20, hivyo mteja kulazimika kurejesha kiasi kikubwa cha fedha tofauti na makubaliano yake na mteja.’’Aliongeza.
Naye Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Mussa Mzee Hussein, amesema Taasisi yake itajielekeza zaidi katika kutoa elimu kwa wafanyabiashara na watumishi wa wa umma ,kutojielekeza katika makapuni yenye kutoa mikopo umiza na ambayo wamiliki wake wana hulka mbaya.
Aidha Hussein amesema Taasisi yake itaendelea kupamba na kuzuia wale wote wanaoendelea na vitendo vya rushwa na kuhakikisha, wanakomesha kabisa ikiwemo kuwachukulia hatua za kisheria kama hawatajiepusha na utoaji mikopo ya chapuchapu ambayo inalenga kutapeli waombaji wa mikopo hiyo.
Mmoja wa waathirika wa mikopo umiza ambaye amerejeshewa kiasi cha shilingi Milioni 18 Mwalimu Mstaafu Elias Katinda, amesema kitendo cha kurejeshewa fedha zake ameamini kwa sasa kuna serikali inayojali wananchi wake na kwamba ana imani kubwa na TAKUKURU.
TAKUKURU itaendelea na zoezi la uchunguzi ili kuwabaini wote waliochukua fedha za wastaafu lakini pia kuwafungulia mashitaka ili iweze kuwa fundisho kwa watu wengine wenye nia mbaya ya kuendelea kuwatepeli wastaafu kupitia mikopo umiza.