NA ABOUD MAHMOUD
TAMASHA la Utamaduni wa Mzanzibari linatarajiwa kufunguliwa rasmi leo ambalo litafanyika Unguja na Pemba.
Akizungumza na Zanzibar Leo,Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa, Sensa, Filamu na Utamaduni (BASSFU) Dk. Omar Abdallah Adam, alisema tamasha hilo linatarajiwa kuanza leo asubuhi kwa burudani ya fensi itakayokusanya vikundi 24.
Alisema burudani hiyo ya fensi inatarajiwa kuanza majira ya saa tatu asubuhi na itaanza Mwanakwerekwe kupitia barabara ya Jang’ombe na kumalizia katika Mnara wa kumbukumbu wa Kisonge.
Katibu huyo alisema baada ya kufika hapo,fensi hiyo inatarajiwa kurudi Mwanakwerekwe kwa kupitia barabara kuu ya Magomeni.
Dk. Omar alisema kuanzia majira ya saa 8:00 mchana hadi 12:00 jioni Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, anatarajiwa kufungua maonyesho ya wajasiriamali yatakayofanyika hapo hapo katika mnara wa kumbukumbu Kisonge.
“Tamasha la Mzanzibari leo tunatarajia kulianza rasmi na litakua la siku nne ambapo burudani mbali mbali zitakuwepo kisiwani Unguja na Pemba,”alisema.