NA KHAMISUU ABDALLAH
TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imetangaza ratiba na tarehe ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar na kuwataka wadau wa uchaguzi kuzingatia katiba na sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid, alisema uchaguzi huo utafanyika Oktoba 28 mwaka huu ukiwa ni wa sita wa mfumo wa vyama vingi vya siasa uliorudishwa mwaka 2012.
Alisema kifungu cha 34(3) na (4) cha sheria ya uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018 inaipa mamlaka tume hiyo kutangaza tarehe na ratiba ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar unaohusisha uchaguzi wa rais wa Zanzibar, wajumbe wa baraza la wawakilishi na madiwani.
Alisema uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi wa wagombea utaanza Agosti 26 hadi Septemba 9 na siku ya uteuzi wa wagombea utafanyika Septemba 10 mwaka huu.
“Kampeni za uchaguzi zitaanza Septemba 11 hadi Oktoba 26, 2020 na siku ya upigaji kura ya mapema itakuwa Oktoba 27, 2020,” alieleza Jaji Hamid.
Mwenyekiti huyo alifahamisha kuwa upigaji kura kwa wananchi wote wa Zanzibar utakuwa ni Oktoba 28 na kura zitaanza kuhesabiwa siku hiyo hiyo hadi Oktoba 31 ambapo matokeo ya uchaguzi yanatarajiwa kutangazwa.
Aidha alisema, ZEC imeamua kutangaza tarehe kufuatia tamko rasmi la kuvunjwa kwa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ambayo ni Agosti 20 mwaka huu.
Akizungumzia utaratibu wa upigaji wa kura ya mapema alisema unafanyika kwa mujibu wa kifungu cha 82 cha sheria ya uchaguzi na kwamba upigaji kura huo utawahusisha watendaji wanaosimamia majukumu ya uchaguzi katika siku ya uchaguzi.
Aliwataja watu hao kuwa ni watendaji wanaosimamia uchaguzi, wakiwemo wasimamizi wa uchaguzi, wasaidizi wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wa vituo, askari polisi watakaokuwa kazini siku hiyo, wajumbe na watendaji wa tume ya uchaguzi na wapiga kura ambao watahusika moja kwa moja na kazi za ulinzi na usalama.
Mwenyekiti huyo aliwaomba wadau wa uchaguzi wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa, waandishi wa habari, vyombo vya ulinzi na usalama, asasi za kiraia na waangalizi wa uchaguzi kuendelea kuhimiza wananchi kudumisha amani na utulivu iliyopo ili waweze kufanikisha uchaguzi huo.
Aidha aliwapongeza wananchi kwa kushiriki katika hatua zote za maandalizi ya uchaguzi huo, kuanzia uandikishaji na uhakiki wa wapiga kura, kufanya mapitio ya idadi, majina na mipaka ya majimbo ya uchaguzi na kazi ya ugawaji wa vitambulisho vya kupigia kura na kuwaomba kuendelea kushirikiana na ZEC katika hatua nyengine za uchaguzi.
Sambamba na hayo aliwasisitiza waandishi wa habari kuendelea kuandika habari za ukweli zitakazowafikia wananchi kwa wakati na kujiepusha kuandika taarifa za upotoshaji ili kuwa na uchaguzi wa amani kama ilivyo kauli mbiu ya mwaka huu isemayo ‘Piga kura yako na dumisha amani ya nchi yako’.
Mapema Mkurugenzi wa uchaguzi wa tume hiyo Thabit Idarous Faina, aliwahimiza wananchi ambao hawajachukua vitambulisho vyao vya kupigia kura, kufika katika ofisi za tume za wilaya zao ili kupatiwa shahada zao.
Alisema ili waweze kushiriki katika hatua ya kupiga kura, watalazimika kuwa na shahada mpya hivyo wale wote waliohakiki na kujiandikisha katika daftari la kudumu na hawakuwahi kuchukua vitambulisho vyao, kufanya hivyo ili kuwawezesha kuwachagua viongozi wanaowataka katika uchaguzi huo.
Ratiba uiliyotangazwa na ZEC inaenda sambamba na ratiba iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wiki mbili zilizopita ambayo iliitangaza oktoba 28 kuwa ni siku ya uchaguzi wa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, wabunge na madiwani.