NA KHAMISUU ABDALLAH

TAASISI ya Viwango Tanzania (TBS) na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), zimesaini hati ya makubaliano yatakayoondosha vikwazo vya kiutendaji baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika Ofisi za Wizara ya Biashara na Viwanda Migombani Waziri wa Wizara hiyo, Balozi Amina Salum alisema makubaliano hayo kwa kiasi kikubwa yatarahisisha biashara na utendaji.

Balozi Amina alisema zimekuwepo changamoto kwa wafanyabiashara wa Zanzibar pale biashara zao zinapoingia katika soko la Tanzania bara ikiwemo suala la usajili wa biashara.

Balozi Amina, alisema pia makubaliano hayo yatakuwa ufunguo kwa wafanyabiashara wa Zanzibar kuendesha biashara zao kwa urahisi na kuweza kukua zaidi.

Alifahamisha kuwa, bado vyombo hivyo vina tofauti kutokana na ZBS kuwa wachanga hivyo aliiomba TBS kushirikiana na taasisi hiyo katika mafunzo mbalimbali ambayo yatawawezesha kufikia walipo.

“Mashirikiano ya dhati kwenu na taasisi yetu katika kuwashirikisha kama taasisi nyengine za muungano basi kwa kiasi kikubwa wataweza kujifunza na taasisi yetu iweze kujifunza,” alisema.

Mbali na hayo, Balozi Amina alisema changamoto ya Tanzania bidhaa bado hazijaweza kupata somo la ithibati katika biashara hivyo ni vyema TBS kuisaidia ZBS kuleta vyombo hivyo ili viweze kusaidia katika majukumu ya kazi zao za kila siku.

Alisema serikali tayari imeshatoa sera ya viwanda na mashirikiano baina ya taasisi binafsi hasa katika kuwasaidia wajasiriamali wadogo wadogo kuona wanakuwa kibiashara ambayo ndio azma ya serikali zote mbili.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Juma Reli, alisisitiza kuwa kuwepo mazingira mazuri ya kibiashara ikiwemo kuondosha urasimu ili kuhakikisha vigezo vinavyowekwa na taasisi za benki ya dunia vinafikiwa na kuifanya Tanzania kuingia katika soko la Afrika Mashariki na SADEC.   

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Yussuf Abdalla, aliahidi mashirikiano hayo yanakuwa na kuhakikisha biashara zinakwenda vizuri na hakuna changamoto ya kibiashara Tanzania kwani nchi hiyo ni moja.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa ZBS Zanzibar, Rahima Ali Bakar, aliishukuru wizara kuiwezesha taasisi hiyo kufikia mashirikiano hayo ili kufikia malengo waliyojiwekea katika utekelezaji wa majukumu yao.